TRC yaanza kupokea mabehewa ya SGR

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limeanza kupokea mabehewa yatakayotumika katika Reli ya Kisasa (SGR).

Mabehewa 14 yaliyotengenezwa na kampuni ya Korea Kusini ya Sun Shin Rolling Stock Technology Limited (SSRST) yamewasili katika Bandari ya Dar es Salaam na kazi ya kuyashusha inaendelea na yatakabidhiwa kesho.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Jamila Mbarouk alisema jana kuwa kampuni hiyo inatengeneza mabehewa 59 yanayogharimu Dola za Marekani 55,645,168.00.

Jamila alisema mabehewa 45 yaliyobaki yanatarajiwa kuwasili Mei mwakani kwa kuwa matengenezo yanaendelea na yamefikia asilimia 86.

Alisema TRC ilisaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya 1,430 ya mizigo kutoka kampuni ya CRRC ya China, mabehewa mapya 59 ya abiria kutoka kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Limited ya Korea Kusini, seti 10 za treni ya kisasa zenye jumla ya mabehewa 80 na vichwa 17 vya umeme kutoka Kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini kwa ajili ya uendeshaji wa SGR.

Jamila alieleza kuwa gharama za mikabata hiyo yote ni Sh trilioni 1.18 na kwamba ipo kwenye hatua za utekelezaji.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea Korea Kusini na kuridhishwa na matengenezo ya mabehewa hayo.

SGR inajumuisha ujenzi wa mtandao wa reli wenye kilometa 1,219 inayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza kukiwa na vipande vitano ambavyo vimefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.

Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 300, mradi unatekelezwa na mkandarasi Yapi Merkezi na umefika 97.19 na unatekelezwa kwa thamani ya Sh trilioni 2.7.

Kipande cha Morogoro -Makutupora kina kilometa 422, kimefika asilimia 87.05 huku kipande hicho kikijengwa kwa gharama ya Sh trilioni 4.4.

Kipande cha tatu cha Makutupora-Tabora kina urefu wa kilometa 368, kipande cha nne ni Tabora-Isaka chenye kilometa 165 na kipande cha Isaka-Mwanza kina urefu wa kilometa 348.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x