TRC,TANAPA kushirikiana kukuza utalii

TRC,TANAPA kushirikiana kukuza utalii

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limesema itashirikiana na  Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kukuza utalii wa ndani, baada ya kutembelea Stesheni ya Mvave iliyopo karibu na mbuga ya Saadani mkoani  Pwani.

Stesheni ya Mvave  iko mbioni kufunguliwa baada ya kukamilika  ukarabati na kwamba itakuwa kichocheo kikubwa   kwa wananchi, pamoja na wageni wanaotumia usafiri wa reli kwenda kutalii katika mbuga  ya Saadani.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara TRC, Never Diamond, amesema  ushirikiano baina ya TRC na TANAPA, unalenga kuangalia miundombinu wezeshi ya kibiashara, kati yao ili kujua jinsi ya kukuza utalii wa ndani kupitia usafiri wa reli.

Advertisement

Diamond amesema kuwa stesheni ya Mvave ni muhimu katika kukuza utalii, hivyo TRC na TANAPA, imeweka mikakati mbalimbali, ambayo itawezesha wananchi kutumia muda wao kwenda kupumzika na kuona vivutio vilivyopo nchini.

“TRC inaunga juhudi za Rais wetu Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii wa ndani na treni ni zaidi ya usafiri kwani ni nafuu na unachochea utalii,” amesema Diamond.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, kutoka  Hifadhi ya Taifa Saadani, Ephraim Mbomo, amesema kuwa kituo cha Mvave kitabadilisha uwezo wa kupokea wageni wanaotumia magari ya kukodisha na kupata huduma ya moja kwa moja kwa kutumia usafiri wa treni.

 

“Treni ni usafiri wa uhakika katika vipindi vyote masika na kiangazi sababu wakati wa masika magari hupata shida kutokana na miundombinu ya barabara. Hifadhi ya Saadani ni hifadhi pekee ambayo mbuga imekutana na bahari,“ amesema Mbomo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *