Treni kutengwa behewa la wazee, wagonjwa
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema anapanga upya njia za usafiri wa treni ijulikanayo kama ‘treni ya mwakyembe’ kwa kuongeza mabehewa ikiwa ni pamoja na kutenganisha behewa la wagonjwa pamoja na wazee.
Chalamila amesema hayo jana alipozungumzia kero ya usafiri katika mkoa wake, mara baada ya kufungua Kongamano la Kimataifa kuhusu utumwa na maisha baada ya utumwa katika historia ya Afrika lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Treni kwa sasa tumefanya utaratibu kuhakikisha tunapanga upya njia zake pamoja na kuongeza mabehewa zaidi pia kutenganisha wagonjwa pamoja na wazee waweze kutumia mabehewa hayo.
“Na kuimarisha barabara ya reli ili kuhakikisha kuwa usafiri huo unaendelea kwa sababu barabara kuu kwa sasa ina foleni kwa sababu tunajenga barabara ya mabasi yaendayo kasi kwa kilomita 20.3 , kwa bilioni 231.5 na barabara hii itakamilika muda si mrefu ili wananchi waweze kutokana na adha hiyo,” amesema.
Amekiri adha ya usafiri ipo kwa sababu ya mvua ambazo zilikuwa zinanyesha na adha hii ya usafiri inapatikana san a maeneo ya kuanzia Chanika, Zingiziwa kuja mpaka Gongo la Mboto na baadhi ya maeneo ya Kivule kwenda mpaka Mwanagati, Kitunda maeneo ambayo hutumia usafiri wa treni kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia mabasi ya mwendo kasi 70 yaliyokuwa yameharibika na kuagizwa yatengenezwe, amesema zaidi ya mabasi 30 yameshatengenezwa.
“Na yale mabasi yalikuwa yameharibika si chini ya 70 yameshatengenezwa mabasi zaidi ya 30 na kumbuka kuwa serikali ina utaratibu wake wa kuondoa mali chakavu kwa hiyo kama mali zile au mabasi yale yatakuwa hayawezi kuingia barabarani kwa mkono wa kiserikali maana yake taratibu ziko wazi yatauzwa kwa njia yam nada ili mabasi mengine yaweze kununuliw,” amesema.
Pia ameongeza kuwa Kwa barabara ya Morogoro inahitaji kuwa na mabasi 177, “ kwa mantiki hiyo naweza kukiri kuwa mabasi yaliyoagizwa mara ya kwanza yaliyokuwa zaidi ya 200 baadhi yake yamechakaa na kwa mantiki hiyo serikali iko kwenye utaratibu kabambe wa kuhakikisha tunapata mabasi ili yaweze kuhudumia wananchi kiasi cha kutosha,” alisema.
Ameongeza kuwa na barabara nyingine ikikamilika mwendo kasi itahitaji mabasi 775, “ maana yake hii nakupa takwimu ndogo sana ili ujue ni usafiri una msongamano mkubwa, umekimbiliwa na watu wengi na rasilimali bado sio nyingi ili kuwachukua watu wanaosafiri kwenye hayo mabasi,”.