Tril 1.2/- kukabiliana na tabianchi

BENKI ya CRDB imekamilisha mchakato wa kupokea fedha Dola za Marekani milioni 500 (Sh trilioni 1.2) za mabadiliko ya tabianchi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo, amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Dk Jafo alisema katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, Ofisi yake iliendelea kuratibu shughuli za Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ulio chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Alisema katika kipindi hicho, Benki ya CRDB imekamilisha mchakato wa kupokea Dola za Marekani milioni 500 pamoja na kusaini mkataba wa usimamizi wa fedha hizo zitakazotumika kwa ajili ya kutoa mikopo na mafunzo kwa wanufaika watarajiwa.

Pia Dk Jafo alisema wizara hiyo inaendelea kuzisaidia taasisi nyingine katika kupata ithibati ya mfuko wa mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Benki za NMB, NBC na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Aidha, alisema ofisi hiyo kwa kushirikiana na Tamisemi imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti ikijumuisha kampeni ya Soma na Mti inayohusisha shule za msingi, sekondari na vyuo.

Alisema kampeni hiyo ya upandaji miti inatekelezwa nchini kwa kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka. “Katika kipindi cha mwaka huu, idadi ya miti iliyopandwa ni milioni 185.6 na iliyostawi ni miti milioni 154.934 sawa na asilimia 83.5,” alisema Dk Jafo. Alisema halmashauri 23 kati ya 184 ndizo zilivuka lango la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.

Habari Zifananazo

Back to top button