Tril 6.7/- kufikisha umeme vitongoji vyote

SERIKALI inatarajia kutumia zaidi ya Sh trilioni 6.7 kugharamia mradi wa kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji vyote 36,101 nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Saidy alisema hayo Morogoro jana katika mkutano wa kwanza wa mwaka kati ya wakala huo na wadau wa maendeleo wakiongozwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Saidy alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 REA imepanga kutumia sh bilioni 784 .84 kati ya hizo Sh bilioni 756.19 ni kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini na Sh bilioni 28.65 ni kwa masuala ya uendeshaji.

Alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 350 zitatoka kwa wadau wa maendeleo.

Saidy alisema lkatika mwaka ujao wa fedha serikali imetenga Sh bilioni 377 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji nchini.

“Kwa sasa tupo kwenye maandalizi na usanifu ili kujua gharama hasili, lakini vitongoji kati ya 2,300 hadi 2,500 vitapata umeme awamu ya kwanza ya mradi huu,“ alisema na kuongeza:

“Unaweza kuona bado tunahitaji rasilimali fedha na moja ya vitu vimezungumzwa katika mkutano wetu na wabia wa maendeleo wanaotufadhili kwa zaidi ya miaka 10 ni kwenye eneo hili kama wanaweza kutusaidia vizuri “.

Saidy alisema serikali imejipanga kuendelea kutekeleza mradi huo kwa awamu hadi kitongoji cha mwisho kipate umeme.

Alisema katika utelekezaji wa mradi wa umeme vijijini unaoendelea wa awamu ya tatu mzunguko wa pili alisema hadi Aprili mwaka huu vijiji 10,129 kati ya 12,345 vimefikiwa na miundombinu ya umeme.

“Huu ni wastani wa asilimia 81 ya vijiji vyote vimefikiwa na umeme na wakandarasi wapo maeneo ya miradi kuweza kuunganisha huduma ya umeme katika vijiji 2,216 zilivyobaki na mpango wetu hadi Desemba mwaka huu viwe vimekamilika na kwa baadhi vitakwenda hadi mwanzoni mwa 2024,” alisema Saidy.

Aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuwa katika miaka mitatu iliyopita walitoa Sh bilioni 659.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janeth Mbene alisema wadau wa maendeleo wameridhishwa na namna REA inavyosimamia fedha wanazoziota na zinazotolewa na serikali.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo, mwakilishi wa ubalozi wa Norway, Kjetil Schie aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuishirikisha sekta binafsi kuchangia shughuli za maendeleo.

Habari Zifananazo

Back to top button