Trump kulipa Dola milioni 350, afungiwa biashara miaka mitatu

MAHAKAMA nchini Marekani imeamuru Rais wa zamani, Donald Trump na kampuni zake kulipa karibu Dola milioni 350 katika uamuzi wa kesi ya ulaghai huko New York.

Trump pia amezuiwa kuhudumu kama ofisa au mkurugenzi wa shirika lolote la New York au chombo kingine cha kisheria katika jimbo hilo kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari *CNN*, Trump anatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Advertisement

Lakini pia taarifa iliyochapishwa usiku huu na gazeti la ‘The *Guardian* la Uingereza limeeleza kuwa uamuzi wa kesi hiyo ni pigo kubwa kwa Trump na himaya yake ya biashara na ushindi mkubwa kwa mwanasheria mkuu wa New York Leticia James, ambaye anatarajiwa kuzungumza juu ya uamuzi huo katika mkutano na waandishi wa habari.

Shirika la Habari la *NBC* la Marekani limesema mbali na faini kubwa na marufuku ya kufanya biashara, Trump pia amezuiwa kupata mikopo kutoka kwa benki za New York kwa miaka mitatu.

Mwanasheria Mkuu wa New York, Letitia James alikuwa akitafuta Dola milioni 370 kutoka kwa Trump, kampuni yake na watendaji wake wakuu, ikiwa ni pamoja na wanawe Donald Trump Jr. na Eric Trump, akidai ni udanganyifu uliorudiwa ambao ulijumuisha kughushi rekodi za biashara na taarifa za kifedha.

James alidai kuwa washtakiwa walitumia taarifa za fedha za uongo kupata mikopo ya benki na sera za bima kwa viwango ambavyo wasingestahili kuvipata na wakavuna mamilioni ya dola kwa njia isiyofaa.

Trump alikuwa ameshikilia kuwa taarifa zake za kifedha zilikuwa za kihafidhina, na ametaja madai ya AG kuwa yamechochewa kisiasa na udanganyifu.