Trump kurejeshwa Facebook, Instagram
Kampuni ya mtandao wa kijamii ya Meta imetangaza kumrejesha aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump kwenye mitandao yake ya Facebook na Instagram, baada ya kufungiwa kwa miaka miwili.
Katika taarifa yao kwenda kwa waandishi wa habari iliyowekwa kwenye tovuti yao, Meta imeeleza kuwa itamruhusu Trump kurejea kwenye mitandao yake badaa ya wiki kadhaa kuanzia sasa.
“Mitandao ya kijamii inatokana na imani kwamba mijadala ya wazi na mtiririko huru wa mawazo ni maadili muhimu, hasa wakati ambapo yanakabiliwa na tishio katika maeneo mengi duniani,” Nick Clegg, rais wa Meta, aliandika.
Hatua hiyo ya kusimamishwa ilipitishwa Januari 7, 2021, siku moja baada ya wafuasi wa Trump kuvamia Ikulu ya Marekani katika jaribio la kuvuruga uidhinishaji wa uchaguzi wa urais wa 2020, ambao chama cha Republican kilishindwa na Joe Biden wa Democratic.
Katika mojawapo ya jumbe zake za mwisho kwenye Facebook kabla ya kusimamishwa kwake, Trump alieneza taarifa potofu kuhusu uchaguzi matokeo kwamba matokeo yalikuwa na udanganyifu.
Pia alitumia jukwaa hilo kumshutumu makamu wake wa rais, Mike Pence, ambaye alikuwa akisimamia uidhinishaji wa kura.