TSN, CRDB zaunganisha nguvu upatikanaji wa habari

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Benki ya CRDB zimekubaliana kuendeleza ushirikiano ili kuongeza upatikanaji wa habari na ujuzi wa huduma za kifedha, uchumi na biashara kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah amesema katika mazungumzo na timu ya viongozi kutoka CRDB kuwa TSN iko tayari kushirikiana na CRDB katika kuandaa majarida ya “Uchumi Wetu” na “Business Standard” kwa HabariLEO na Daily News mtawalia.

“Kuna maeneo mengi tunayotegemea kushirikiana zaidi. Eneo la uandaaji wa majarida ya Elimika, Academy na Wanawake. Tunafanya uchapishaji wa kibiashara na kwenye eneo la habari, TSN tuna uzoefu wa tangu miaka ya 1930,” amesema Tuma.

Ujumbe wa CRDB uliongozwa na Mkurugenzi wa Manunuzi, Pendason Philemon. CRDB inajivunia kutengeneza faida ya Sh bilioni 424 na ongezeko la asilimia 23 la utoaji mikopo sawa na Sh trilioni 8.9 kutokana na mahusiano mazuri na vyombo vya habari, pamoja na mambo mengine.

Benki hiyo kubwa nchini imesema imekuwa ikitoa mitaji kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu na inaamini Ushirikiano na vyombo vya habari unaongeza uelewa wa huduma za kifedha na ufikiaji wananchi kupitia bidhaa mbalimbali zinazotolewa na benki.

Habari Zifananazo

Back to top button