TSN kujiimarisha kidijiti, mauzo kuongezwa 30%
WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imelieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imepanga kuunganisha mifumo wezeshi ya kiutendaji ikiwemo ya fedha, biashara na utawala kuwa ya kidijiti.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema bungeni Dodoma jana kuwa katika mwaka huo, TSN imepanga kutekeleza shughuli saba.
Nape alisema TSN imepanga kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma zitolewazo na kampuni kwa asilimia 30 na kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha uchapaji na kufunga mitambo ya kisasa ya uchapaji.
Alisema pia TSN imepanga kuendesha programu nne za mafunzo na kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu habari za kiuchunguzi na uandishi wa kitakwimu.
Nape alisema pia TSN imepanga kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za serikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kuunganisha taasisi na mashirika kwenye huduma ya magazeti mtandao.
Alisema pia TSN imepanga kutekeleza mpango kabambe wa kuhabarisha umma kupitia magazeti yake ya Daily News, HabariLEO na mitandao yake ya kijamii kuhusu utekelezaji wa shughuli za serikali kuanzia mwaka 2020.
Alisema TSN imepanga kukusanya Sh 26,831,676,908.00 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya uendeshaji wa kampuni na ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Isome:https:https://habarileo.co.tz/tsn-yaanza-ujenzi-studio-ya-kisasa/
Alisema hadi Aprili mwaka huu TSN imeendelea na ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kufunga mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji ambao ujenzi umefikia asilimia 35.
“Aidha, kampuni imepokea jumla ya mitambo mipya ya kisasa mikubwa minne pamoja na mitambo midogo saba ambayo ni sehemu ya mitambo mikubwa. Kwa ujumla mitambo hiyo iliyopokelewa ina thamani ya shilingi 15,749,232,000.43,” alisema.
Nape alisema kampuni hiyo imeongeza wauzaji na mawakala wapya wa magazeti wanane katika mikoa ya Dar es Salaam (3), Tanga (2), Kilimanjaro (1) na Morogoro (2).
Alisema pia TSN imeongeza wateja binafsi 80 na kampuni tano walionunua magazeti mtandaoni hivyo kufanya jumla ya wateja binafsi kufikia 1,354 na kampuni 34 mtawalia.
Alieleza TSN imekamilisha uundaji wa programu tumizi ya simu inayotarajiwa kuongeza idadi ya watumiaji wanaojisajili kusoma habari na magazeti ya TSN mtandaoni.
“Kampuni inafanya mapitio ya mwisho ya programu hiyo kabla ya kuanza kutumika rasmi kabla ya Julai, 2024,” alisema Nape.
Alisema TSN imetoa ushauri na huduma za kihabari kwa taasisi, imefanya mazungumzo yenye lengo la kukuza ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi zikiwemo wizara, taasisi na mashirika ya umma, vyombo vya habari, balozi na taasisi za kimataifa.
Alisema taratibu za ukamilishwaji wa makubaliano ya utoaji wa huduma za ushauri wa kihabari zinaendelea kati ya TSN na Wizara ya Kilimo; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi); Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC); ofisi za wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Lindi na Mtwara na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Wengine ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Wakala ya Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Nape alisema TSN imeanza ujenzi wa studio ya kisasa na ununuzi wa vifaa vya studio na imenunua magari sita kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa majukumu ya kampuni.
Alisema kampuni hiyo imeanza kutekeleza programu ya mahojiano na viongozi wastaafu ijulikanayo kama ‘Former Leaders Bench with Daily News”.
“Jumla ya viongozi 12 wakiwemo Makamu wa Rais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu, maspika wastaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar wamefanyiwa mahojiano kwa lengo la kutoa mitazamo yao juu ya uongozi wa nchi hii kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa pamoja na kutoa elimu juu ya historia na masuala mbalimbali yanayohusu taifa kwa ujumla,” alisema Nape.