TSN yaanza ujenzi studio ya kisasa

DODOMA: KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN), imeanza utekelezaji wa ujenzi wa studio ya kisasa na ununuzi wa vifaa vya studio kwa ajili ya habari za kidigitali.

Hayo yamesemwa bungeni na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2024/2025 kwa wizara yake leo Mei 16,2024 jijini Dodoma.

Soma pia: https://habarileo.co.tz/nape-amtaka-katibu-mkuu-kuongeza-nguvu-ujenzi-tsn/
“Mheshimiwa Spika, Hadi Aprili, 2024 Kampuni imetekeleza majukumu yafuatayo, Kuendelea na ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kufunga mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 35.

“Aidha, Kampuni imepokea jumla ya mitambo mipya ya kisasa mikubwa minne (4) pamoja na mitambo midogo saba (7) ambayo ni sehemu ya mitambo mikubwa. Kwa ujumla mitambo hiyo iliyopokelewa ina thamani ya shilingi 15,749,232,000.43…

“Kukamilisha uundaji wa Programu Tumizi ya simu ambayo inatarajiwa kuongeza idadi ya watumiaji wanaojisajili kusoma habari na magazeti ya TSN mtandaoni. Kampuni inafanya mapitio ya mwisho ya programu hiyo kabla ya kuanza kutumika rasmi kabla ya Julai, 2024;

“Kutoa ushauri na huduma za kihabari kwa taasisi mbalimbali. Aidha, Kampuni imefanya mazungumzo yenye lengo la kukuza ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi zikiwemo wizara, taasisi na mashirika ya umma, vyombo vya habari, balozi na taasisi za kimataifa.

“Kuanza ujenzi wa studio ya kisasa (multimedia studio) pamoja na ununuzi wa vifaa vya studio. Kuanzisha na kutekeleza programu maalum ya mahojiano na viongozi wastaafu ijulikanayo kama ’Former Leaders Bench with Daily News,” amesema Waziri Nape.

Soma pia: https://youtu.be/HFznwEhYZzk?si=fQplzhBPwaUMg8nh

Habari Zifananazo

Back to top button