TTB, Njombe waipangia mikakati hifadhi ya Kitulo

BODI ya Utalii nchini (TTB), imepanga kuinua utalii uliopo Nyanda za Juu Kusini, husuani mkoa wa Njombe katika hifadhi ya Kitulo, ikiwa ni kuendeleza program ya kukuza utalii nchini kupitia ya filamu ya Royal Tour.
Hifadhi hiyo ina aina mbalimbali za maua zaidi ya 200, lakini pia ikiwa na utalii mkubwa wa ndege kuhama kutoka Njombe kwenda Ulaya na kurejea tena.
Kaimu Mkurugenzi wa TTB, FeliX John, amesema hayo leo Dar es Salaam, wakati akielezea uzinduzi mkakati na maonesho ya vivutio vya utalii vya eneo hilo, yatakayoanza kesho Septemba 25 na kilele chake kuwa Septemba 27, ambayo ni siku ya utalii duniani.
Amesema wajibu wa Bodi hiyo ni pamoja na kuongeza vivutio vya utalii nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa filamu ya Royal Tour, kukiwa na lengo la kufikia idadi ya watalii milioni tano, kufikia mwaka 2025.
Kuhusu maonesho ya utalii Njombe, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kupitia maonesho hayo wanaiambia dunia kuwa hifadhi ya Kitulo ni maalum na ya kipekee, ikisheheni maua ya aina mbalimbali.
Amewataka wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo, hususani katika eneo la hoteli na kwamba ardhi ipo ya kutosha na yenye kuhimili hali ya hewa iliyo nzuri kwa kipindi chote.