DAR ES SALAAM; Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limejipanga kufanya upanuzi wa mkongo wa Taifa ili kuongeza mawasilino hadi upande wa magharibi wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga amesema hayo leo Dar es Salaam katika ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Khamis Abdullah kukagua vifaa vya upanuzi wa mkongo awamu ya tatu sehemu ya pili.
Amesema upanuzi huo wa mkongo unatekelezwa na TTCL kwa kushirikiana na mkandarasi, ambapo wilaya 32 zitaunganishwa na mkongo huo, huku wilaya tisa kati ya hizo ujenzi wake ukifanywa na TTCL na wilaya 23 zilizobakia zikijengwa na mkandarasi.
Amesema kukamilika kwa upanuzi huo utawezesha wilaya 100 kufikiwa na mkongo huo kati ya wilaya 139 zilizopo nchini na zilizobakia zikitarajia kukamilika kabla ya Desemba 2024 .
Ulanga amesema katika upanuzi huo vituo tisa vitajengwa na wataalam wa ndani na tayari maandalizi mbalimbali yamefanyika kwa ajili ya utekelezaji na kwa upande wa mkandarasi malipo yameshafanyika na mkataba umeanza rasmi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Abdallah ameziagiza taasisi pamoja na mashirika binafsi ambayo hayajapeleka taarifa zake katika Kituo cha Taifa cha kuhifadhi Data kufanya, hivyo kwa kuwa ni sehemu salama na inayotosheleza.
Amesema kituo cha kuhifadhi data ambacho kinasimamiwa na TTCL, kina usalama wa kutosha, kina ulinzi na kinalindwa hivyo taasisi zikiwemo wizara mbalimbali ziende kuweka taarifa zao hapo.
Kuhusu upanuzi wa mkongo ameitaka TTCL kutambua kuwa serikali imeiamini hivyo isiiangushe katika kuhakikisha upanuzi huo unafanyika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa kwa kuwa inalenga kufika katika uchumi wa kidijtali.