‘Tuangalie athari za mfumuko wa bei, tusiishie kulaumu’

‘Tuangalie athari za mfumuko wa bei, tusiishie kulaumu’

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, amewataka wananchi mkoani Kagera kuangalia sababu na vyanzo vya mfumuko wa bei za bidhaa nchini ikiwemo vyakula badala ya kulaumu serikali.

Ameyasema  hayo wakati akiwahutubia wananchi  katika hafla maalum iliyofanyika Uwanja wa Mayunga,Manispaa ya Bukoba ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi alizozifanya na anazoendelea kuzifanya mkoani humo na Tanzania kwa ujumla tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.

“Ndugu zangu lazima kwanza tuangalie athari za kiuchumi, ambazo zilijitokeza wakati Raisi Samia anaingia madarakani, baadhi ya watu wamesikika wakiwa wanalalamikia kupanda kwa bei ya vyakula na watu hawa wakiwa wanaendelea kuhusisha uongozi wake bila kufanya uchunguzi wa sababu maalumu.

Advertisement

“Wakati Rais anaingia madarakani ugonjwa wa UVIKO 19 ndiyo kwanza umeanza kuingia na athari zake kiuchumi zilikuwa kubwa sio hapa nchini duniani kote, kwani uzalishaji haukuwepo viwandani, watu hawakulima,  vyakula havikupata masoko haya yote yamesababisha kupanda kwa bei za vyakula nchini, “alisema Chalamila

Alisema sababu nyingine ni pamoja na vita vya Ukraine na urusi, ambavyo kimsingi vimeathiri uchumi wa mataifa yote ulimwengini, ikiwemo Tanzania, lakini Rais Samia aliendelea kusimama hasa katika kuleta mbolea za ruzuku, ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuangalia kama bei ya vyakula inaweza kushuka.

Pia amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi yalisababisha mvua chache nchini suala lililofanya wakulima kupata mavuno hafifu.

Aisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia, Mkoa wa Kagera umepokea fedha nyingi za ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa haijawahi kutekelezwa mkoani humo tangu nchi ipate uhuru, hususani miradi ya maji, afya, elimu, barabara pamoja na nishati.

“Tumepokea fedha nyingi katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, awali tulipata madarasa 881 yaliyotumia zaidi ya Sh bil. 17 na awamu ya pili ililetwa zaidi ya Sh bil.10 zilizotumika kujenga madarasa madarasa 514.

“Tumefanikiwa kujengewa shule 12 zenye hadhi zilizogharimu  Shbil.8, uanzishwaji wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tawi la Kagera, zaidi ya  Sh bilioni  40 zimetumika katika ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya katika kila halmashauri,” alisema.

Alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera kuendelea kumuunga mkono kwa vitendo, kufanya kazi kwa bidii, kuendelea kuzalisha chakula kwa wingi, kulima kilimo chenye tija ili msimu wa mavuno ukifika waweze kuchangia uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla .