SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limeishukuru serikali kwa kuongeza mishahara kwa wafanyakazi nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo Mei 5, 2023 na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Said Wamba na kusema kuwa wamefurahishwa na maamuzi yaliyofikiwa akiamini kuwa huo ni mwanzo mzuri.
Amesema wamekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na serikali ambayo ni endelevu hivyo wataendelea kufikisha mahitaji mengine ikiwemo kutazama upya mfumo wa kodi ili nyongeza inayotolewa iwe na tija kwa wafanyakazi.
Wamba akawageukia wafanyakazi na viongozi wa wafanyakazi, kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ari na ufanisi unaotakiwa, ili kuwaongezea nguvu viongozi wa vyama kudai stahiki zao.
Katika mazungumzo yake hayo yaliyochukua dakika zisizozidi 20, Wamba anafafanua kuwa vyama vya wafanyakazi haviko kwa ajili ya mapambano, bali ni majadiliano katika kumsaidia mfanyakazi.
Mei 1, 2023 ilikuwa ni siku ya wafanyakazi Duniani, ambapo kwa Tanzania iliadhimishwa kitaifa mkoani Morogoro mgeni rasmi akiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.