TUCTA yakoshwa ushiriki wa NBC maadhimisho Mei Mosi

Arusha: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jana imeungana na maelfu ya wafanyakazi kote nchini kusherekea Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani,  ambayo kitaifa yamefanyika jijini Arusha yakiongozwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango aliemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo, yalipambwa na uwepo wa washiriki wengi zaidi wakiwemo viongozi mbalimbali wa kiserikali, kidini, vyama na shirikisho la wafanyakazi huku Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na wakubwa wa benki ya NBC Elibariki Masuke akiwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo kushereheka siku hiyo muhimu.

Akizungumzia maadhimisho hayo Masuke alisema mbali na ushiriki huo benki ya NBC ni miongoni mwa wadhamini wakubwa wa maadhimisho hayo yanayoratibiwa na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo vyama mbalimbali vya wafanyakazi.

“Katika maadhimisho haya NBC tunaungana na maelfu ya wafanyakazi wenzetu kote nchini kusheherekea siku hii muhimu sana kwa wafanyakazi, kwanza tukiwa kama wafanyakazi, pili tukiwa wadhamini muhimu katika kufanikisha uratibu wa maadhimisho haya na zaidi tunashiriki kama watoa huduma za kifedha kwa wafanyakazi kupitia matawi yetu yaliyopo kote nchini,’’ alisema.

Kwa mujibu wa  Masuke benki hiyo imekuwa na utamaduni wa kudhamini maadhimisho hayo kwa miaka mingi sasa kutokana na kutambua umuhimu wake kwa wafanyakazi ambao ni nguzo muhimu katika ustawi wa benki hiyo kupitia huduma mbalimbali za kibenki inazozitoa kwa wafanyakazi hao.

Habari Zifananazo

Back to top button