Tuhakikishe watoto wanapata chanjo ya polio

Tuhakikishe watoto wanapata chanjo ya polio

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuanza Kampeni ya Awamu ya Tatu ya kutoa matone ya chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kuanzia leo Septemba Mosi hadi 4, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio inafanyika kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea Malawi, Februari 17 na kisha Msumbiji, Mei mwaka huu.

Ummy ameeleza kuwa kampeni hiyo itakuwa ni kwa nchi nzima na katika awamu hii ya tatu wamelenga kuwafikia watoto 12,386,854 walio chini ya umri wa miaka mitano.

Advertisement

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kuwa unapotokea mlipuko au tishio la mlipuko wa ugonjwa wa polio nchini, nchi husika na nchi jirani zipaswa kufanya kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa awamu nne mfululizo.

Takwimu za Wizara ya Afya zimeonesha kuwapo kwa mafanikio makubwa katika awamu zilizopita ambazo awamu ya kwanza ya kampeni iliwafikia watoto 1,130,261 sawa na asilimia 115 ya watoto wa umri huo katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma na Njombe ambayo inapakana na nchi ya Malawi.

Katika awamu ya pili iliyofanyika nchi nzima kuanzia Mei 18 hadi 21, mwaka huu, iliwafikia watoto 12,131,049 sawa na asilimia 118.8.

Haya ni mafanikio makubwa na inaonesha kuwapo kwa mwitikio mkubwa kwa wananchi kupeleka watoto hao wa umri wa chini ya miaka mitano kupata chanjo ya polio.

Virusi vya polio huathiri mfumo wa neva na huweza kusababisha udhaifu wa misuli au kupooza. Athari zake huweza kusababisha ulemavu wa kudumu na vifo. Chanjo imepunguza uwepo wa virusi hivi katika nchi nyingi. Watu ambao hawajapata chanjo wapo kwenye hatari ya kuambukizwa.

Kutokana na hali hiyo, tunaamini jamii itaona umuhimu wa kupeleka watoto kuchanjwa na kuachana na imani potofu za baadhi ya watu kuhusu chanjo mbalimbali zinazotolewa na serikali kuwakinga watu wake.

Ni kwa msingi huo tunawaomba wazazi na walezi wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano kutumia siku hizi nne kuanzia leo kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya ugonjwa huo ambao ni hatari kwa watoto wadogo.

Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kuhakikisha inapata chanjo za magonjwa mbalimbali yakiwamo yale yanayowakabili watoto kama polio, surua na mengineyo, hivyo ni wajibu wa wananchi kutumia fursa hizo kuwakinga watoto wao na magonjwa husika.

Itakuwa ni jambo la kushangaza endapo watoto hawatapatiwa chanjo hii hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya nchi jirani zimepata mlipuko wa ugonjwa huo, hivyo kama wanavyosema Waswahili kinga ni bora kuliko tiba.

Tuwapeleke watoto chini ya umri wa miaka mitano wakapate kinga hii ili tuwaepushe na polio, kwani serikali inawajali wananchi wake na ni wajibu wa wananchi nao kutocheza na afya za kizazi hiki cha baadaye.