‘Tujiandae kwa fursa AFCON 2027’

DODOMA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka Watanzania kujiandaa na fursa mbalimbali kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2027 kwa pamoja nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Pia Waziri Mkuu amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika michezo, ulioiwezesha Tanzania iwe juu na kutambulika kimataifa katika masuala ya kimichezo, hali ambayo imefanya pia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mpira wa miguu kushika namba tano kwa ubora Afrika, huku michezo mingine nayo Tanzania ikitamba.

SOMA: Mikakati yaanza kusukwa AFCON 2027

Advertisement

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Makete Festo Sanga, wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu, aliyehoji kutokana na jukumu kubwa lililopo mbele kuandaa fainali hizo, kwa nini serikali isiweke mkakati wa fedha za gawio na CSR zikaelekezwa katika kitu kama Mfuko Maalum kwa ajili ya fainali hizo, ili zitumike katika ujenzi wa viwanja na maandalizi mengine yahusiyo michezo hiyo.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema ni ushauri ambao wizara yenye dhamana ya michezo imeusikia na wataufanyia kazi kwani tayari maandalizi kuhusiana na fainali hizo yameshaanza, ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba wa ujenzi wa uwanja mkoani Arusha na baadaye utajengwa mwingine mkoani Dodoma.

SOMA: Uwanja mpya Arusha kutumika PAMOJA AFCON 2027

Pia amesema ukarabati wa viwanja mbalimbali utafanyika katika mikoa mbalimbali nchini, hivyo kusisitiza wananchi kujiandaa na fursa mbalimbali za kibiashara kwa mashindano hayo kufanyika hapa nchini, ikiwemo malazi, vyakula, vinywaji, usafiri na mengineyo.

/* */