‘Tujipange viwanda vya bidhaa zinazotokana na madini’

TANZANIA inapaswa kuwa na viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazotokana na madini, ili kuchochea ukuaji wa pato la taifa.

Kamishna Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini, anayeshughulika na Usimamizi wa Mazingira, Ally Samaje amesema hayo wakati wa mafunzo ya usimamizi wa kodi kwenye sekta ya madini.

Akizungumza hayo katika mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), Samaje amesema kwa kuwa na viwanda maana yake ni kwamba vitalipa kodi na kuajiri Watanzania, hivyo manufaa yatakuwa makubwa.

“Huko mbeleni ili tuhakikishe kuwa tunanufaika zaidi ni lazima tuhakikishe kuwa tunavutia viwanda vinavyotumia rasilimali madini katika kutengeneza bidhaa za mwisho.

“Kwa mfano sasa hivi sisi tuna uchimbaji wa Nickel utaanza kule Kabanga, watachakata kule, na kuleta makinikia Kahama watachakata mpaka kupata bidhaa ambazo zinazoenda kutumika kwenye viwanda mfano vya kuzalisha betri.

“Kwa hiyo manufaa tutakayopata hapa ni tofauti na jinsi ambavyo tungeishia kwenye makinikia tukasafirisha nje makinikia sasa tumeongeza hatua mbele, tukienda hatua nyingine sasa kunakuwa na viwanda vinavyotengeneza betri kutokana na Nikel maana yake sasa tumepata yale manufaa yanayotokana na madini haya,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa yale madini yanayosafirishwa nje ya nchi serikali inapaswa kukamata mnyororo mzima wa thamani kuanzia yanapochimbwa na kuchakatwa mpaka mwisho ndipo taifa litanufaika.

Meneja wa Afrika Mashariki wa Asasi ya Utawala wa Rasilimali (NRGI), Moses Kulaba amesema wanashirikiana na serikali kuhakikisha sekta ya uziduaji ina manufaa kwa nchi ambazo zina rasilimali zikiwemo madini, gesi na mafuta.

Amesema kwa kuwa madini imekuwa ni sekta ya kimkakati kwa nchi, inabidi mafunzo yatolewe kuhusu usimamizi wa kodi kwenye sekta hiyo.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, serikali inapaswa kujipanga kuandaa mifumo sahihi ya kuhakikisha hata ikipita kipindi hicho, uchumi utasimama imara huko sekta hiyo ikizalisha kodi ya kutosha kuhakikisha wananchi wananufaika.

Amesema ukitoa sekta ya utalii inayofuatia ni ya uziduaji, lakini ili nchi ifikwe kwenye malengo yake na kuwa ya uchumi wa kati angalau sekta hiyo ingefikia asilimia 10 tofauti na ilivyo sasa asilimia 6.7.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Repoa, Lucas Katera amesema mafunzo hayo yanawajengea uwezo watafiti na wafanyakazi katika sekta mbalimbali zinazoendana na rasilimali za nchi.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button