Tukaze uzi udhibiti usafiri wa wanafunzi

JUMATATU ijayo Januari 8, mwaka huu, muhula wa kwanza wa masomo utaanza kwa shule za awali, msingi na sekondari kote nchini.

Ni wakati mwingine ambao pilikapilika zinakuwa nyingi kuanzia kwa wazazi, walimu hadi kwa wenye kusimamia sekta nzima ya elimu na zile mtambuka.

Mojawapo ya changamoto zinazojitokeza sasa, ni suala la usafiri kwa wanafunzi wa shule hizo hasa wale wanaoishi mijini wanaohitaji usafiri kuwafikisha na kuwarudisha maeneo ya shule zao.

Kwa muda sasa, baadhi ya shule hasa zile za binafsi zimekuwa na huduma yao ya usafiri, lakini kwa wanafunzi wengine wamekuwa wakitumia usafiri wa umma kwenda shule na kurudi nyumbani.

Hawa wamekuwa wakikabiliwa na adha kubwa kwani vyombo vingi vya usafiri vimekuwa vikiwakataa kuwachukua kwa visingizio mbalimbali.

Hali hiyo imewafanya wachelewe kufika shuleni na pia kurudi nyumbani, hivyo kusababisha mara nyingi wanafunzi kuzorota katika suala la masomo kwani wanachelewa kufika shule na pia wanachelewa kufika nyumbani, hali ambayo si nzuri.

Lakini pia zipo shule zenye mabasi yao binafsi, na nyingi ni zile za binafsi. Hata hivyo, mabasi haya yamekuwa na changamoto ikiwamo ya ubovu, kujaza wanafunzi kupita kiasi na usimamizi hafifu kiasi cha kuwapo madai ya vitendo vya udhalilishaji kutoka kwa madereva au makondakta.

Haya yote pamoja na sababu nyingine, yamezua tatizo jingine mijini ambako wanafunzi wakiwamo watoto wadogo, wanapelekwa shuleni kwa kutumia usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda, hali ambayo inawaweka watoto katika hatari kubwa.

Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani kimepiga marufuku matukio haya yote ya kujaza wanafunzi kupita kiasi katika magari, kuwasafirisha watoto kwa bodaboda na magari kusafirisha wanafunzi pasipo kukaguliwa.

Ni imani yetu kwamba wakati shule zinapofunguliwa Jumatatu ijayo, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani pamoja na mamlaka nyingine hasa zile zinazoshughulikia usafiri, litatekeleza wajibu wao kuhakikisha magari mabovu, yasiyokaguliwa, yanayojaza wanafunzi kupita kiasi, na yale yanayokataa kuwabeba, yanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

Hii itasaidia kuhakikisha watoto hawa wanakuwa salama wakati wote wanapokwenda na kurudi shule, kwani kiujumla, usafiri wao umekuwa na changamoto nyingi zenye hatari kwa watoto hawa.

Tunaamini trafiki na vyombo vingine hawajashindwa katika jukumu hili kiasi cha wenye magari haya ya shule na yale ya kutoa huduma kwa umma, yaonekane yameshindikana kudhibitiwa, hivyo kufanya mambo yao wanavyotaka wao.

Na hili ni muhimu hasa wakati huu ambao jamii inalalamika kuhusu mmomonyoko wa maadili ambao miongoni mwa waathirika wakubwa ni watoto.

Hivyo tuchukue hatua kali sasa kuwalinda watoto hao na majanga yanayoweza kuepukika. Tusisubiri hadi hali iwe mbaya zaidi, hatujachelewa lakini pia hatuwezi kuendelea kufumbia mambo au kutoa matamko, hatua zinapaswa kuonekana zinachukuliwa, tena hatua kali ambazo zitakuwa fundisho kwa wengine wenye tabia hizo.

Pia ni muda mwafaka serikali sasa kuanza kufikiria kuweka bajeti za kununua magari ya wanafunzi kwa shule za serikali hasa maeneo ya mijini kupitia halmashauri zake.

Habari Zifananazo

Back to top button