KATIKA jamii yetu kumekuwepo na wimbi la matukio ya kuuana kwa wapenzi au wanandoa kutokana na sababu mbalimbali kuanzia wivu wa mapenzi hadi imani za kishirikina.
Matukio haya yamekuwa yakiongezeka kila uchwao huku yakiteketeza watu ambao ni tegemeo katika familia zao na taifa kwa ujumla.
Hali hiyo imekuwa ikiacha familia hasa watoto katika wakati mgumu kutokana na kuhitaji malezi ya wazazi wote wawili.
Mauaji ya wenza yamekuwa yakiripotiwa huku yakiongezeka na wanawake ndio wamekuwa walengwa wakubwa. Mwaka 2021 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliripoti kwamba katika matukio 35 wanawake walikuwa 31, sawa na asilimia 89 huku wanaume wakiwa wanne.
Kwa mujibu wa LHRC, matukio ya ukatili dhidi ya wanawake kutoka kwa wenzao ndani ya mwezi Mei pekee mwaka huu yalikuwa saba.
Mbali na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, pia kumekuwa na wimbi la ukatili dhidi ya watoto hususani utesaji, vitendo vya ulawiti na ubakaji lakini pia matukio ya mauaji yameripotiwa.
Hii inadhihirisha kwamba kumekuwa na ukiukwaji wa mila, desturi na miongozo ya dini kwani haya yote yanahimiza maadili mema, upendo na upole. Ukiangalia watu wengi wanaohusika katika matukio haya si wapagani kwa maana kwamba wanaamini katika dini ambazo zinakataza mambo haya.
Hali hii inaonesha kwamba jamii ina kila sababu ya kujitazama upya na kuangalia wapi inakosea ili kurekebisha hali hii kwa kuzingatia mila na desturi sambamba na mafundisho ya dini. Je, viongozi wa dini wanafanya kazi yao sawia katika kujenga jamii yenye hofu na Mungu?
Je, wazazi wanatoa malezi bora kwa watoto wao kwa kuwajengea msingi mzuri wa kuwa wanajamii waungwana na wema kwa kila mtu? Je, jamii yenyewe inachangiaje kuharibika kwa maadili? Je, utandawazi una mchango wake katika haya?
Lakini, imekuwa ikielezwa kwamba ukatili huu umekuwa wakati mwingine ukitokana na imani za kishirikina. Je, katika karne hii ni kwa nini bado Watanzania wanaamini ramli chonganishi na utapeli wa baadhi ya waganga wa jadi?
Kwa nini jamii imekuwa nzito katika kutafuta suluhu yanapotokea matatizo kwenye ndoa au kwa wapenzi. Je, hakuna wazee, viongozi wa dini na vyombo vya sheria ili kuepusha majanga kunapotokea changamoto katika ndoa?
Wanandoa kabla ya kuingia katika jukumu hilo wanapata mafundisho sahihi kutoka kwa wazazi, makungwi na hatimaye viongozi wa dini?
Inaelezwa kwamba kuna tatizo pia la kisaikolojia miongoni mwa wanajamii linalochangia ukatili huu.
Bila shaka ni muhimu sasa maswali hayo yakatafutiwa majibu na wanafamilia, wazazi, wazee wa mila, viongozi wa dini na serikali kwa ujumla. Katika suala la saikolojia hivi karibuni serikali iliahidi kuanza kuchukua hatua kwa kutoa elimu shuleni hadi mitaani.
Yanabaki hayo mengine. Kila kunapotokea ukatili, ni vyema ufanyiwe utafiti kujua sababu na kutafuta ufumbuzi ili kukomesha ukatili huu ambao kwa sasa unaongezeka kila kukicha na kuelekea kuonekana kama kitu cha kawaida katika jamii.