‘Tulidanganywa Msomera kuna ushirikina tusiende’

BAADHI ya wananchi katika Hifadhi ya Ngorongoro walidanganywa wasiende Msomera, Handeni kwani kuna ushirikina ikiwa ni pamoja na mawe ya ajabu ambayo ukiyakanyaga unajikuta upo nje ya nyumba yako.

Akizungumza na HabariLEO, kijana wa kimasai anayeishi Kijiji cha Esere, Kata ya Alaitole ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Isaya Liomomo anaelezea kuwa baadhi ya watu wakiwemo wanaharakati wenye mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) , waliwahadaa kwa kuwaeleza kuwa Msomera si mahali salama kuishi kwa sababu ya imani za kishirikina.

Hata hivyo anasema walishangaa kwani awali waligoma, lakini walipowasiliana na wenzao ambao wapo Msomera, ambao wamepewa nyumba na  maeneo yenye hatimiliki, hawakausikia tena kauli za kichawi, bali walielezwa fursa za kimaendeleo zilizopo.

“Awali tulidanganywa tukienda Msomera tukikanyanga mawe tu yanaongea au ukilala unajikuta upo katikati ya pori lenye nyoka wengi, lakini kadri siku zinavyoenda hakuna kitu kama hicho, waliopo huko hawasemi mambo ya ushirikina, ” amesema.

Liomomo anasema yeye ni kijana anayetegemewa na ndugu zake zaidi ya kumi na kazi kubwa anayofanya nje ya Ngorongoro ni ulinzi katika baadhi ya maeneo na kuuza viatu mbalimbali.

“Nimechoka kulinda nyumba za watu niliposikia zoezi la kujiandikisha nilijiandikisha sasa nasubiri serikali ituhamishe na wenzangu wengine hapa kijijini tukaendelee na maisha yetu huko Msomera, hapa hakuna jambo lolote linaloendelea la kimaendeleo kwa sababu ya uhifadhi sasa sioni faida ya kuteseka nataka uhuru wangu,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button