Tulisimama kwenye treni Dar hadi Mwanza!

HAIKUWA jambo la ajabu kuwa safarini zaidi ya wiki kwa usafiri wa treni kutokana na changamoto za hapa na pale.

Treni ndio ulikuwa usafiri wa wengi kati ya Dar es Salaam na Kigoma na Mwanza pamoja na mikoa mingine ambayo Reli ya Kati ilipita.

Kwa wanafunzi waliokuwa wakitoka mikoa hiyo, watakumbuka walivyopewa mabehewa maalumu huku wakitumia waranti kipindi cha kwenda na kutoka likizo.

Mwandishi wa makala haya, Stella Nyemenohi

Kwa wale tuliofika Mwanza na kulazimika kuendelea na safari ya majini katika Ziwa Victoria, waranti hiyo hiyo ilitumika kwani kipindi hicho cha miaka ya 1988 hadi 1997 Shirika la Reli Tanzania lilisimamia pia usafiri wa meli.

Enzi hizo meli kutoka Mwanza kwenda Bukoba zilikuwa Mv Victoria, Mv Butiama, Mv Serengeti na Mv Bukoba.

Acha niendelee kukueleza usafiri wa treni na yaliyojiri enzi hizo!

Wanaofahamu usafiri wa daladala na msongamano ndani ya mabasi hayo, wanaweza kunielewa.

Mathalani, mkoani Dar es Salaam yapo maeneo ambayo ni nadra kuona daladala bila abiria waliosongamana kiasi cha mtu kusimama kwa mguu mmoja.

Hivi ndivyo naweza kuelezea usafiri wa treni enzi hizo katika Daraja la tatu takribani miaka 30 iliyopita.

Fikiria safari ya zaidi ya siku moja umesimama kwenye treni huku kukiwa na msongamano wa watu mithili ya daladala za Dar es Salaam!

Abiria waliobahatika kupata nafasi uvunguni mwa viti, walilazimika kujikunja kama si kulala! Wengine walikaa juu ya viti miguu ikining’inia mabegani mwa abiria waliokuwa na ‘siti’.

Chooni pia hapakuwa na faragha kwani wapo abiria waliolazimika kukaa eneo hilo na wengine wakisimama eneo la maungio ya mabehewa ilimradi wafike waendapo.

Kusafiri kwa treni daraja la tatu na hasa kipindi cha likizo za wanafunzi, kulitawaliwa na adha za hapa na pale. Wizi wa mizigo haukuwa kitu cha ajabu katika baadhi ya stesheni.

Stesheni ya Tabora (mjini) ilikuwa miongoni mwa maeneo ambayo abiria walichukua tahadhari kubwa kutokana na kutajwa kuwa na vitendo vingi vya wizi wa mizigo.

Wizi haukuishia daraja la tatu bali pia madaraja mengine (ya kulala). Ukijisahau, vibaka waliingia kupitia madirishani, wakaiba na kutokomea.

Abiria walipeana taarifa za kila mmoja kuwa macho na mizigo ikizingatiwa ilikaa Tabora muda mrefu kutokana na mchakato wa kutenganisha mabehewa ya kwenda Kigoma/Mpanda na mengine kwenda Mwanza.

Ilikuwa jambo la kawaida kwa abiria kufungasha vyakula na maji ya kunywa njiani. Ikumbukwe enzi hizo hapakuwapo na wigo mpana wa vyakula vya njiani wala maji ya chupa kama ilivyo sasa. Usipobeba maji, basi tegemea kununua maji ya kwenye ndoo yaliyochotwa visimani.

Mkoa wa Dodoma ulikuwa maarufu kwa biashara ya maji. “Aaa maji, maji ya kunywa” zilisikika sauti za wachuuzi wengi wakiwa wanawake waliokuwa wakishawishi abiria kununua maji hayo yenye tope.

Kwa upande wa chakula, abiria walitegemea kununua chakula cha njiani. Eneo la Saranda mkoani Singida lilikuwa maarufu kwa kitoweo cha kuku.

Treni ilikuwa ikisimama kwa takribani dakika tano ili watu wapate chakula. Nakumbuka wali kwa mchuzi wa kuku, uliosheheni binzari. Ililazimu kula ‘kijeshi’ hasa treni ilipopiga king’ora kuashiria kuondoka.

Hata hivyo, pamoja na hekaheka zote, haiondoi ukweli kwamba usafiri wa treni una raha yake. Ni usafiri wa kuvinjari.

Treni ninayozungumzia ni ya Reli ya Kati yenye historia ndefu.  Ipo njia ya Dar es Salaam kwenda Kigoma iliyojengwa mwaka 1905 hadi 1914 wakati huo Tanganyika ikiwa koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Mwaka 1919 Serikali ya Uingereza ilianzisha mamlaka ya Huduma za Reli na Bandari ya Tanganyika ambayo iliongeza njia ikiwamo kutoka Tabora hadi Mwanza, iliyofunguliwa mwaka 1928.

Sasa reli hii inayoendeshwa chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ina mabadiliko makubwa yaliyofanya Jicho Langu liwaze nchi ilikotoka hadi sasa hasa kwa kuangazia usafiri kuanzia miaka ya 1980.

Nikakumbuka mwaka 1997 pale usafiri wa maji (Ziwa Victoria) ulivyotengwa na wa reli na huduma ya reli ilivyoendelea kushuka huku kukiwa na majaribio kadhaa za kuifufua.

Kwa msaada wa machapisho mbalimbali, nikakumbuka mwaka 2006 Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilivyovunjwa na umiliki wa njia za reli ukapewa kampuni ya Reli Assets Holding Company Ltd Rahco.

Kisha shughuli za kuendesha usafiri wa reli zikahamishiwa kwa shirika jipya la Tanzania Railways Limited (TRL) iliyokuwa mradi wa pamoja kati Serikali ya Tanzania na kampuni ya Rites kutoka India.

Baadaye mwaka 2011 Serikali ya Tanzania ikachukua hisa zote za TRL. Mtandao wa reli ukabaki mkononi mwa serikali na mwaka 2017 TRC ikafufuka tena, huduma zikaanza kuboreka.

Aprili 2017 ulianza mradi wa reli ya kisasa (SGR). Awamu ya kwanza ya ujenzi ulianzia Dar es Salaam mpaka Morogoro, umbali wa kilometa 300. Pia Morogoro-Makutupora (Dodoma).

Mwanza

Wakati treni ya Reli ya Kati pia ikiendelea kutoa huduma, sasa gumzo ni reli ya kisasa.

Taarifa ya TRC ya hivi karibuni kuhusu maendeleo ya mradi wa SGR awamu ya kwanza inasema umefikia asilimia 98.90 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro chenye kilometa 300. Kipande cha Morogoro hadi Makutupora maendeleo ya mradi yamefikia asilimia 96.51.

Vipande vingine na asilimia zake kwenye mabano ni Makutupora hadi Tabora (13.98), Tabora-Isaka (5.44) na Mwanza-Isaka (54.01).

Wakati huo huo seti ya kwanza ya treni ya kisasa inayojumuisha vichwa vitano vya umeme na mabehewa matatu ya abiria, iliwasili hivi karibuni.

Katika taarifa yake kwa umma, TRC inasema seti nyingine zinatarajiwa kuendelea kuwasili kila mwezi hadi Oktoba 2024.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali kupitia TRC ilifanya ununuzi wa seti 10 za treni ya kisasa zinazojulikana kama Electric Multiple Unit (EMU) kutoka kwa watengenezaji wa kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini.

Seti moja ina uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.

EMU inatajwa kuwa ni treni iliyoundwa kwa teknolojia ya kisasa inayomwezesha abiria kupata huduma muhimu ikiwamo huduma ya mtandao (Wi-Fi), sehemu za kukaa watu wenye mahitaji maalumu, mifumo ubaridi na kamera za usalama (CCTV).

Hatua ya TRC kupokea mabehewa 65 ya abiria, vichwa tisa vya umeme, seti moja ya EMU na kuwasili kwa vitendea kazi, kunafanya nchi kuwa tayari kuanza huduma za usafirishaji abiria katika reli ya kiwango cha kimataifa.

Hakika nchi inasonga. Zile safari za siku zaidi ya tatu njiani, msongamano ndani ya behewa na mzigo kichwani, sasa ni yamebaki kuwa hadithi za kale kwamba: “Hapo zamani za kale tulisafiri tukiwa tumesimama kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza”.

 

Back to top button