Tumbaku inaingiza Dola 182 kwa mwaka
UZALISHAJI wa zao la tumbaku nchini Tanzania unawezesha taifa kupata Dola milioni 182 kila mwaka.
Meneja Mkuu wa Chama Kilele cha Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Tumbaku Tanzania, Benedict Kisaka amesema hayo wakati wa Mkutano wa 35 wa Umoja wa Wakulima wa Tumbaku Duniani uliofanyika mkoani Dar es Salaam.
“Zao la tumbaku ni moja ya mazao matano ya kimkakati katika kujenga uchumi wa Tanzania, na tukumbuke Tanzania zao la tumbaku linalimwa na wakulima takriban milioni mbili na nusu na uzalishaji unatupatia dola za marekani milioni 182 kila mwaka.
“Kama zao la kuuzwa nje ya Tanzania na uchumi wetu unategemea sana kilimo bora na ndio maana katika mkutano tunazungumzia namna ya kuboresha uendelevu wa uzalishaji na kilimo bora cha tumbaku Tanzania,” amesema.
Amesema uzalishaji umekuwa ukiboreshwa kila mwaka kwa kuwa mwaka 2021/22 kilo milioni 62 za tumbaku zilizalishwa, mwaka 2022/23 kilo milioni 138 zilizalishwa na matarajio katika msimu ujao wa mwaka 2023/24 wanatarajia kuzalisha kilo Sh milioni 212.
Amesema dhamira kuu katika mkutano huo ni kuongelea suala la kilimo endelevu cha tumbaku pamoja na kuzungumzia maandalizi ya mkutano wa Novemba ambao ajenda mojawapo itakuwa hali ya kutokuwa na mlingano katika sheria zinazowabana wakulima wa tumbaku kwenye kuendeleza zao hilo.
“Kwa sauti moja tutaangalia namna gani tunaweza kuelewa sera na sheria zilizowekwa kumlinda mkulima na zile zilizoletwa na Shirika la Afya Duniani na FTCC kuhusu namna ya kuweza kupunguza jitihada za kuongeza uzalishaji wa zao la tumbaku,” amesema.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu Umoja wa Tumbaku Duniani, Mercedes Vazqez amesema katika uzalishaji wa tumbaku inapaswa kuwa makini katika suala la kimazingira na kijamii.
Amekiri tumbaku sio nzuri kwa afya ila wanafuata maelekezo, sera ya uzalishaji wa tumbaku.
Katika Mkutano huo wa 35 wa umoja wa wakulima wa tumbaku duniani Tanzania ndiye mwenyeji, nchi nyingine zilizohudhuria ni Argentina, Brazil, Bulgaria, India, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Poland, Ureno,Afrika Kusini, Marekani na Hispania.