Tumbaku yampeleka Diamond Chunya
MSANII Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, atakonga nyoyo za wakulima wa Tumbaku wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kupitia tamasha la Sauti ya Mkulima Wakati ni Sasa.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco Ltd yenye makao yake makuu mjini Morogoro.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ahamed Huwel amesema tamasha hilo linalolenga kuhamasisha kilimo cha tumbaku wilayani humo na nchini kwa ujumla litafanyika Jumapili wiki hii katika kata ya Lupatingatinga wilayani humo.
Pamoja na kuongeza hamasa ya kilimo hicho cha kibiashara kinachoweza kuinua uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla, Huwel amesema tamasha hilo litatumika pia kutoa elimu ya madhara ya ajira za watoto mashambani, ili wasikose haki zao ikiwemo ya elimu.
Diamond mwenyewe amewataka wakulima hao pamoja na wananchi wengine wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo la mkulima lisilo na kiingilio.
“Itakuwa mara yangu ya kwanza kufika na kutumbuiza Lupa Tingatinga, naomba wakulima na wapenzi wangu wote jitokezeni kwa wingi, tuimbe, tucheze na tufurahi pamoja katika kupaza sauti ya mkulima wa Tumbaku,” alisema.
Diamond atashiriki tamasha hilo ikiwa ni siku kadhaa zipite toka msanii wa lebo yake Zuchu kutumbuiza katika jimbo la Nsimbo mkoani Katavi kulikofanyika uzinduzi wa masoko ya Tumbaku ya msimu wa mwaka huu.
Wakati wa uzinduzi huo, kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco Ltd iliahidi kununua kilo milioni 265 za tumbaku katika misimu mitatu ya soko hatua inayotarajiwa kupeleka furaha kwa wakulima na kusaidia kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo nchini.
Wakati kilo milioni 45 zinatarajiwa kununuliwa msimu huu na kampuni hiyo nchini kote, Huwel alisema watanunua kilo milioni 90 msimu unaofuta na kilo milioni 130 msimu wa tatu.