TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa yake kuhusu mfumo wa sheria unaosimamia makosa dhidi ya maadili hapa nchini.
Wakili wa Serikali kutoka katika tume hiyo, Ismail Hatibu amesema hayo katika maonesho ya Kitaifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale Mkoani Mbeya.
Hatibu amesema hakuna asiyefahamu hivi sasa kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili hapa nchini na kutolea mfano suala la vijana kujiingiza katika masuala ya ushoga, ubakaji, ulawiti, unyanyasaji wa kijinsia, usagaji pamoja na madanguro.
Amesema mmonyoko huo wa maadili umekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini.
“Sisi kama tume ya kurekebisha sheria tuko katika hatua za mwisho kukamilisha ripoti yetu ili kutoa maoni na mapendekezo yetu nini kifanyike ili kuweza kukabiliana na changamoto hii inayotukabili kwa sasa hapa nchini,” amesema.
Kwa upande mwingine alisema tume hiyo imekuwepo katika maonesho hayo ya wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwa imeshatoa ripoti yake kuhusiana na mfumo wa sheria inayosimamia mazao ya masoko ya kilimo nchini Tanzania.
“Sasa katika sheria hii tumeishauri serikali na tumetoa mapendekezo yetu kwamba sasa hivi yako mazao ya biashara yanayotambulika na kusimamiwa na bodi mbalimbali, kwa mfano kuna bodi ya pareto, bodi ya mkonge, tumbaku, kahawa, na nyinginezo.
“Sasa unaona bodi hizi zinasimamia mazao haya kama mazao ya biashara na moja ya majukumu yao ni pamoja na kupata masoko ndani na nje ya nchi , lakini sisi kama tume tumeona yapo mazao ambayo ni ya chakula lakini leo ni mazao ya biashara,” amesema.
Alitolea mfano mpunga, mahindi, parachichi na machungwa kuwa ni mazao ya biashara, hivyo wameshauri serikali kwa kutoa mawazo yao ili kupitia mapendekezo yao ione ni namna gani ya kuwasaidia wakulima wapate soko zuri katika mazao hayo.
“Kwa sababu hawa wanalima mazao yao kule mashambani vijijini, mazao mengine yanaharibika kule shambani, lakini pia wanalanguliwa hawapati soko zuri.
“Kwa hiyo tumetoa maoni yetu na mapendekezo yetu kwa serikali ni namna gani serikali inaweza kuwasaidia wakulima hawa kupata soko zuri katika mazao yao,” amesema.
Alisema serikali imeshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na kutolea mfano stakabadhi ghalani inamsaidia mwananchi aliyelima mazao yake kuyaweka ghalani kupitia mazao yale mkulima anaweza akachukua mkopo.
Lakini kupitia mazao yale inasaidia mfanyabiashara kwenda kununua mazao yale.
Alisema maoni hayo wanayoyapeleka serikalini wanayapokea kutoka kwa wadau, hivyo kama tume inayawasilisha serikalini na serikali inayafanyia kazi.
Comments are closed.