Tume yapingwa kuondoa ukamataji kwa ma-RC, ma-DC

WASOMI na wachambuzi wa masuala ya siasa wameshauri wakuu wa mikoa na wilaya wasiondolewe mamlaka ya kuwakamata na kuwaweka mahabusu watuhumiwa wa uhalifu.

Pia, wameshauri Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na vyama vya siasa hasa chenye serikali iliyo madarakani, wahakikishe kila kiongozi anayeteuliwa anazingatia maadili ya uongozi.

Tume ya kuangalia namna ya kuboresha taasisi za hakijinai imependekeza Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97 irekebishwe ili kuondoa mamlaka ya ukamataji waliyonayo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine kwa nafasi zao.

Advertisement

Muhtasari wa ripoti ya tume hiyo umeeleza kuwa endapo ni muhimu kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kuwa na mamlaka ya ukamataji, viongozi hao waelekezwe kuwa wanapotekeleza mamlaka hayo kupitia vifungu vya Saba na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97 mtawalia, wazingatie masharti.

Tume ilitaja baadhi ya masharti hayo kuwa ni kosa liwe linatendeka mbele yake, liwe kosa la jinai ambalo mtu anaweza kushtakiwa, kosa litakalokuwa limetendwa liwe limesababisha kuvunjika kwa amani na utulivu na hakuna namna ya kulizuia kutendeka.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia na Mchambuzi wa Masuala ya Diplomasia na Siasa, Abbas Mwalimu alisema suala si kuondoa mamlaka ya viongozi hao ila kuhakikisha viongozi hao wanatii na kuzingatia uadilifu, sheria, taratibu na kanuni zilizopo.

Aidha, Mwalimu alihimiza kuwe na sheria ya kuwadhibiti wanaokwenda kinyume na mamlaka yao ili wasitumie madaraka yao vibaya kuumiza wengine.

“Hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema uhuru bila mipaka ni vurugu. Ukiacha bila kuweka udhibiti ni vurugu maana yake kila mtu anajifanyia jambo lake. Viongozi wawe waadilifu wajikite zaidi kushirikiana na wasaidizi wao ili kufanya watu waelewe wajibu wao na mipaka ya wajibu wao,” alisema Mwalimu.

Alisema wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wakiondolewa mamlaka hayo inawezekana likatengenezwa bomu lingine kwa kuwa vyombo vya dola hasa polisi hawafiki kila sehemu tofauti na viongozi wa umma.

“Hatuna mtandao wa kutosha kutoa haki jinai nchini. Mfano polisi maeneo mengi wanafanya kazi mwisho saa 12 jioni, mtu anafanya uhalifu saa nne usiku mpaka utafute polisi ni kazi kubwa, wapo polisi jamii lakini hawako sehemu zote,” alieleza.

Alisema ipo Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo kwa sasa kazi yake kubwa inayoonekana ni kusimamia mali za viongozi, inatakiwa itoe elimu kwa viongozi wa umma na kuwachukulia hatua wale wanaokiuka taratibu za uongozi.

“Mifumo ya kiutumishi, Tume (Sekretarieti) ya Maadili, na chama cha siasa (CCM yenye viongozi madarakani), ifanye kazi ipasavyo ili kuwaongoza hawa viongozi wafanye kazi kwa kufuata taratibu. Tume pia ifanye kazi ipasavyo, inataja tu mali lakini hatujaona viongozi wakichukuliwa hatua wanapotumia vibaya madaraka yao,” aliongeza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) na mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Mwigamba alisema bado kuna umuhimu wa kuyaacha madaraka hayo kwa wakuu wa mikoa na wilaya.

“Kuna wahalifu wengine wamejificha ndani ya utumishi wa umma, biashara na shughuli za kijamii ambao si rahisi askari polisi kuwang’amua na kuwakamata kwa makosa ya jinai. Ma-RC na ma-DC wanapowang’amua wawe na mamlaka ya kuwasweka ndani, itasaidia kuwatisha na kupunguza uhalifu,” alisema Mwigamba.

Alisema wakuu wa mikoa na wilaya wasipokuwa na mamlaka ya kukamata watuhumiwa, kutakuwa na athari katika utoaji haki.

Alisema viongozi wakuu wa kitaifa hupita kwenye mikoa na wilaya mara chache, lakini ma-RC na ma-DC wapo kwenye maeneo hayo muda mwingi, na ni rahisi kukutana na maovu na kero na kuchukua hatua haraka.