Tume yataka uchunguzi mali zilizotaifishwa

TUME ya kuangalia namna ya kuboresha taasisi za haki jinai imependekeza iundwe timu kuchunguza utata katika baadhi ya mali zilizotaifishwa katika utaratibu wa vikosi kazi na mashauri ya kukiri kosa ili kuishauri serikali ipasavyo.

Katika muhtasari wa ripoti ya tume hiyo, pia imependekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) itunze kumbukumbu za majadiliano ya makubaliano ya kukiri kosa.

Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, pia imependekeza malalamiko ya washtakiwa kulazimishwa kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa yashughulikiwe kwa njia ya mahakama kwa mujibu wa sheria.

Pia imependekeza elimu zaidi itolewe kwa wananchi na wadau kuhusu utaratibu wa kukiri makosa ya jinai.

Makubaliano ya kukiri makosa ya jinai ni utaratibu wa kumaliza kesi za jinai mahakamani kwa njia ya makubaliano.

Katika utaratibu huo, mshitakiwa anakubali kukiri kosa analoshtakiwa nalo au kosa dogo miongoni mwa makosa aliyoshtakiwa nayo au kwa makubaliano na mwendesha mashtaka kumshtaki kwa kosa dogo au kosa lenye adhabu ndogo.

“Utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa unafanyika katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Marekani, Afrika Kusini, India, Ufilipino, Kenya na Zambia,” ilieleza taarifa ya muhtasari wa ripoti ya tume hiyo.

Tume ilieleza kuwa utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa nchini unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura 20, Tangazo la Serikali Namba 180 la Mwaka 2021, Notisi ya Ugatuzi wa Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Mwaka 2024 na Mwongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Makubaliano ya Kukiri Kosa wa Mwaka 2022.

Muhtasari huo ulieleza kuwa utaratibu wa kukiri kosa unahusisha hatua kuu tatu ikiwamo ya kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kuingia makubaliano ya kukiri kosa, marekebisho ya hati ya mashtaka na kusainiwa na kuusajili mahakamani mkataba wa kukiri kosa.

Tume ilieleza kuwa ilipokea maoni ya wadau kuhusu utekelezaji wa utaratibu wa kukiri kosa na ikabainishwa kulikuwa na uchelewaji wa mashauri kumalizika kwa utaratibu huo kwa kuwa ridhaa ya DPP haikupatikana kwa wakati.

Ilibainika kuwa ucheleweshaji huo ulitokana na washtakiwa kulazimishwa kuingia mikataba ya kukiri makosa bila hiari na kutokuwepo uwazi kwa kuwa mashauri ya kukiri kosa nchi nzima kushughulikiwa na DPP na timu ya maofisa wanne.

Tume ilieleza kuwa malalamiko yaliyotolewa na wadau yalitokana na mfumo wa kisheria uliokuwepo hasa katika awamu ya kwanza na ya pili ya utekelezaji wa utaratibu huo kwa kuwa sheria ilianza kutekelezwa bila kuwapo kanuni zinazoelekeza utaratibu mahususi wa kuzingatiwa na mamlaka ya DPP kutogatuliwa mikoani na kwa maofisa wengine.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x