Tume yaundwa kuchunguza kifo cha aliyefia Polisi

RC Geita, Martin Shigella

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema kuwa kamati maalumu imeundwa kuchunguza kifo cha mkazi wa Mganza wilayani Chato, Enos Msalaba (34) mtuhumiwa aliyefariki mikononi mwa polisi.

Shigella alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kamati hiyo inahusisha wajumbe wa kamati ya usalama ya mkoa ili kupata kiini halisi cha tukio.

Alisema hatua hiyo imekuja kufuatia taharuki iliyojitokeza na kupelekea ndugu kugoma kuzika mwili wa marehemu na wananchi kwenda kuchoma kituo cha polisi Mganza wakidai polisi wamehusika.

Advertisement

Shigella alisema vyombo vyote vya usalama vya mkoa ndio vimeunda kamati ya uchunguzi ili kupata ukweli na kuepuka dhana ya kulindana kwenye Jeshi la Polisi na kumaliza taharuki iliyojitokeza.

Alithibitisha katika polisi kujihami kwa bahati mbaya wananchi wanne walijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya kanda Chato, mmoja akiwa kitengo cha wagonjwa mahututi.

Akizungumza juzi na wananchi waliohudhuria msiba wa Enos kijijini Mganza, alisema jopo la madaktari kutoka nje ya Mkoa wa Geita tayari wamefika kijijini hapo kuchunguza mwili wa marehemu.

Alisema wameagiza wataalamu kutoka nje ya mkoa na kuongeza kuwa kuna madaktari kutoka Dar es Salaam waliofika kufanya uchunguzi, kujiridhisha chanzo cha kifo hicho kama kinafanana na kile kilichoelezwa.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa italinganisha taarifa ya ripoti ya pili itakayotolewa na ile ya kwanza na kuweka wazi chanzo cha kifo cha marehemu na kuruhusu hatua za kisheria kwa wahusika.

Shigella aliwataka wakazi wa Mganza na mkoa mzima wa Geita kuzingatia misingi ya sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi ili kuepuka kuibua taharuki na kusababisha machafuko yasiyo ya lazima.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay alithibitisha Kituo cha Polisi Mganza kuchomwa moto na kugoma kuzika mwili wa marehemu huyo aliyekuwa anashikiliwa kwa wizi wa betri.