‘Tumeendelea kudhibiti ugonjwa wa virusi vya marburg’

WIZARA ya Afya imesema inaendelea kudhibiti ugonjwa uliosababishwa na virusi vya marburg na kuua watu watano mkoani Kagera, ambapo mpaka sasa hivi hakuna mgonjwa mpya aliyeongezeka.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa mpaka  leo Machi 25, serikali inaendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa 3 na inaendelea kufatilia wahisiwa 205 waliotengamana na wagonjwa, ikiwa 89 wanatoka idara ya Afya, ambapo mwanzo serikali ilikuwa inafuatilia wahisiwa 193.

“Tumefikia kuwafuatilia watu 205 na wote hawa wanatoka katika familia za wagonjwa  na watu waliofariki pamoja na wahudumu wa afya ambao walikutana na wagonjwa.

“Ikiwa siku ya 9 tangu kutokea kwa ugonjwa huo, hatujapata taarifa ya uwepo wa mgonjwa au dalili za ugonjwa na tunaendelea kuwashikilia  wahisiwa,” alisema Waziri Ummy.

Alisema timu ya wataalamu wa afya kutoka Wilaya ya Muleba, wamekodi meli kwa ajili ya kutembelea kisiwa cha Goziba, ambapo ndipo mgonjwa wa kwanza alipotokea na  timu hiyo itafanya uchunguzi juu ya nini kilitokea pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya tahadhari za kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema kwa sasa kuna mafunzo ya afya  yanatolewa kwa wahudumu ngazi ya jamii wapatao 1,322, ambao watafanya kazi ya kutoa elimu kwa jamii kwa kipindi cha miezi mitatu juu ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Aliwaondoa wasiwasi wananchi wa mkoani Kagera kuhusu Ugonjwa huo na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari, bila kusitisha shughuli zao za uzalishaji.

Mwakilishi mkazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO),  Dk Zablon Yoti,  alisema amefurahishwa na ushirikiano wa huduma zinazotolewa na tahadhari katika viwanja vya ndege na bandarini katika wilaya ya Bukoba, juu ya mlipuko wa ugonjowa huo na kusema kuwa WHO linauchukulia ugonjwa huo kama kitu kinachohitaji huduma ya haraka.

Alisema kinachohitajika ni umoja na ushirikiano katika idara za afya wa kufanya ugonjwa usienee, lakini pia kuhakikisha wahudumu wa afya wanalindwa kwa nguvu zote, kwani wao ndio mstari wa mbele kuhakikisha wagonjwa wanabaki salama.

Habari Zifananazo

Back to top button