TUMERAHISISHA: Huduma ya mikopo kwa wanawake kidijitali yazinduliwa

Benki ya Equity imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa kuzindua kampeni iliyojikita  kutoa suluhu kidigitali katika huduma zake kwa wanawake.

Kaulimbiu ya kimataifa ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ya mwaka huu ni “Ubunifu na Teknolojia zinatumika kufikia Usawa wa Kijinsia”.

Wakati dunia ikiadhimisha siku hiyo kwa namna mbalimbali, benki hiyo iliungana na wadau wengi kwa kuzindua kampeni ya “TUMERAHISHA” yenye lengo la kuwawezesha wateja wake  kupata huduma za benki za kidigitali kwa urahisi zaidi.

Kwa lengo la kumsaidia mwanamke, benki hiyo imeanzisha huduma ya mikopo kwa njia ya  kidigitali ambayo inaondoa haja ya kwenda moja kwa moja benki kupata huduma hiyo.

“Wenye akaunti za vikundi pia wanaweza sasa kupata huduma zao kupitia simu zao za mkononi.

Aidha, tunatoa mikopo ya kilimo kusaidia wanawake katika kuboresha kilimo chao na kugeuza kuwa biashara yenye faida ili kujiunga kiuchumi,” imesema taarifa ya benki hiyo.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake ni maadhimisho ya mafanikio ya kijamii, kiuchumi, kitamaduni na kisiasa ya wanawake, pamoja na wito wa kuchukua hatua za kuongeza kasi ya usawa wa kijinsia.

Faida za usawa wa kijinsia sio tu kwa wanawake na wasichana bali kwa kila mtu ambaye maisha yake yatabadilika kutokana na dunia yenye usawa.

“Mwaka huu, lengo kuu ni kusherehekea wanawake na wasichana ambao wamebadilisha teknolojia katika sekta mbalimbali, ikiwemo benki, kote ulimwenguni. Benki ya Equity iko mstari wa mbele katika mapambano ya kuhakikisha huduma zao zote zinadigitilizwa,” imeongeza taarifa hiyo.

Benki hiyo inajivunia kuwa miongoni mwa taasisi chache za kifedha zinazoongozwa na na Mkurugenzi Mtendaji mwanamke, jambo linalochukuliwa kama hatua kwani imeonesha kwa vitendo kuwa “mwanamke anaweza.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button