‘Tumieni fursa ya msamaha kusalimisha silaha haramu’

SERIKALI imewataka wananchi wote wanaomiliki silaha  kinyume cha sheria, watumie fursa ya msamaha kusalimisha silaha wanazozimiliki isivyo halali.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini wakati kizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Hamad Masauni  kwenye uzinduzi wa mwezi wa msamaha wa Afrika wa kusalimisha silaha haramu kwa hiyari nchini Tanzania.

Alisema kuwa wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sharia, wajitokeze kusalimisha silaha hizo.

Alisema serikali imekuwa ikiunga mkono, mikakati ya Jumuiya ya Kikanda na Kimataifa katika kupambana na tatizo la uzagaaji wa silaha haramu.

“Katika kutekeleza mpango huu, Serikali imetangaza msamaha wa kutoshtakiwa kwa mtu yeyote, ambaye atasalimisha silaha anayoimiliki isivyo halali kuanzia Septemba  Mosi  hadi  Oktoba 31, mwaka huu  na utafanyika katika vituo vya Polisi, ofisi za Serikali za Mitaa/Vijiji na kwa Mtendaji wa Kata,” alisema.

Alisema kuwa mtu yeyote atakayepatikana na silaha haramu baada ya kipindi cha msamaha kuisha, atachukuliwa hatua za kisheria kama wahalifu wengine.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali litaendesha kampeni ya kitaifa inayolenga usalimishaji wa silaha haramu kwa kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba, 2022.

“Kampeni hii ni fursa ya kuonesha muendelezo wa dhamira ya Tanzania katika masuala ya amani na usalama barani Afrika, ikizingatiwa kuwa kwa sasa Tanzania ni Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika,” alisema

Habari Zifananazo

Back to top button