‘Tumieni majukwaa wezeshi kujiinua kiuchumi’

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima

WANAWAKE na vijana wametakiwa kutumia majukwaa wezeshi ya wajasiriamali, ili kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo na kuepuka mikopo ya kausha damu.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amesema hayo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya wajasiriamali yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala 2023 yakiwalenga zaidi wanawake na vijana kupitia mpango wa Imbeju.

“Wanawake na vijana tumieni haya majukwaa wezeshi ya wajasiriamali ili kujikwamua kiuchumi na kuwainua wenzenu walioko huko majumbani ambao hawaelewi fursa zipo wapi, pia achaneni na mikopo ya kausha damu na wawezeshi na wao waachane na mikopo ya kausha damu na wajiunge na mikopo ya Imbeju kwa sababu haina riba na twende  tukawaambie wewe unakaushwa damu kwa nini?  Twende Imbeju,” alisema Gwajima.

Advertisement

Amesema wanawake na vijana ndio uchumi wa Taifa la Tanzania, kwa sababu kundi hilo lina uwezo mkubwa wa kuinua nchi kwenye mafanikio ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Ripoti ya sensa ya mwaka 2022 inaonesha asilimia 51 ya watu wote nchini ni wanawake na asilimia 75 ni vijana, Taifa lisipoendelea lazima tuwaulize wanawake na vijana kuna changamoto gani kutokana na nafasi na wingi wao katika taifa ili tuzifanyie kazi wapate njia ya kupita tupate kuendelea,” alisema.

Gwajima alisema hata hivyo inaonesha nguvu kubwa ya taifa ipo kwa wanawake na vijana lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo mila na desturi kandamizi, elimu duni, ukosefu wa mitaji na ustadi wa ujasiriamali, ndio maana serikali ilizitambua changamoto hizo na imechukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto zinazolenga kujenga uchumi jumuishi na shirikishi, ili kuwakomboa wanawake na vijana.

Alisema serikali imejitoa kwa dhati kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi ndio maana wanaendelea kufanya kazi kwa bidii kufikia Jukwaa la kimataifa la kukuza usawa wa kijinsia, hususani haki na usawa wa kiuchumi.

Alisema moja ya malengo ya jukwaa ni kuzitambua changamoto za wajasiriamali wanawake na vijana katika kukua kiuchumi, aliwapongeza CRDB kwa kutambua uelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Aliwataka Watanzania kushiriki katika majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake na vijana ili kupata fursa mbalimbali zitakazowawezesha kujiunua kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo imejikita katika sera ya kuinua uchumi wa makundi maalumu, ikiwemo kundi la wanawake na vijana kwa kuwawezesha kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo mitaji, elimu ya ujasiriamali, kuwawezesha wanawake kuweka fedha zao katika sehemu salama.

Alisema katika sekta ya kuinua wanawake, benki hiyo imetoa sh trilioni 3.4 ambazo zimenufaisha wanawake zaidi ya 200,000, sehemu kubwa ya fedha hizo ni kuwawezesha elimu na mitaji.

Baadhi ya vijana wakifuatilia mada kwenye moja ya mikutano waliyoshiriki. (Picha ya Maktaba).

Alisema moja ya changamoto katika kuliwezesha kundi hilo ilikuwa ni jinsi ya kuwafikia na kujua mipango na mawazo yao ya biashara na wengi wao kuogopa wakidhani kuna riba ndio maana walianzia na elimu.

“Mradi ya Imbeju imekuja kutatua changamoto za wanawake na vijana, hivyo wachangamkie fursa hii na tutaendelea kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakuwa wafanyabiashara wakubwa na wenye kuzalisha bidhaa bora za mikono yao na ni kitu ambalo kitainua na kukuza pato la nchi kwa sababu mradi wa Imbeju pia inatengeneza walipa kodi bora,” amesema.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema wilaya hiyo itjitahidi kuwapatia masoko wajasiriamali hao na jitihada hizo zitakuwa sambamba na malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wanawake na vijana.

“Mpaka Juni 2023 imepatikana mikopo zaidi ya Sh Bilioni 27 katika Wilaya ya Ilala kwa zaidi ya vikundi 2063 vimenufaika, lakini vikundi hivyo baada ya kupewa mikopo hiyo vimeweza kufanya marejesho ya asilimia 10 zaidi ya Sh bilioni 17.9,” alisema Mpogolo

4 comments

Comments are closed.