‘Tumieni mbolea kuvuna zaidi’
KIGOMA: WAKULIMA nchini wametakiwa kutumia mbolea kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ili kukifanya kilimo kuwa na tija kubwa hivyo kuondokana na kilimo cha mazoea na kufanya kilimo kuwa biashara yenye tija kubwa.
Meneja masoko wa Kampuni ya Mbolea ya Minjingu, Dk Mbete Mshindo Msolla amesema hayo katika mafunzo kwa mawakala wa mbolea kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga na Singida kuhusu usimamizi wa rutuba ya udongo na matumizi bora ya mbolea yaliyokuwa yakitolewa na Minjingu.
Dk Msolla amesema kuwa kutokana na uhaba wa ardhi watanzania wameondokana na kilimo cha kuhamahama na kwa sasa wanalima eneo moja ambalo limekuwa linachoka na hivyo kushindwa kutoa tija ya kutosha kwenye kilimo na kwamba kuondokana na tatizo hilo matumizi ya mbolea yamekuwa na tija kubwa kukifanya kilimo kuwa na uzalishaji mkubwa.
Amesema kuwa matumizi ya mbolea yanapaswa kwenda sambamba na matumizi sahihi na wakati husika wa kalenda ya kilimo na kwamba mkulima akitekeleza hayo kilimo kinayo nafasi kubwa ya kuinua uchumi wa Maisha ya wananchi wa kawaida vijijini.
Akifungua mafunzo hayo, Ofisa Kilimo kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma, James Peter amesema kuwa Mkoa wa Kigoma umeanza kupiga hatua kubwa ya kuondokana na changamoto ya mbolea kushindwa kufika kwa wakulima na kuchelewa kufika kwa wakulima kulingana na kalenda ya kilimo.
Peter amesema kuwa msimu wa kilimo uliopita mkoa ulikuwa na mawakala watano wa mbolea ya ruzuku jambo lililokuwa changamoto kubwa kwa wakulima kutopata mbolea hiyo na kwamba mwaka huu serikali ya mkoa imeongeza mawakala na kufikia 56 na kuwepo kwa vituo 64 hivyo mbolea ya ruzuku imeweza kufika kwa wakulima wengi na kwa wakati hivyo tathmini kuonyesha kuwa mkoa Kigoma utakuwa na nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.