‘Tumieni ujuzi mliopata wanafunzi wapende fizikia’

WALIMU 26 wa sekondari wa somo la fizikia kutoka shule 13 za serikali jijini Dar es Salaam, wametakiwa kutumia ujuzi, maarifa na mbinu mbalimbali walizozipataza kuwawezesha wanafunzi waelewe na kulipenda somo hilo, ili  kuongeza ufaulu.

Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kalanja ametoa wito huo, wakati wa hitimisho la mafunzo kwa walimu hao yaliyoandaliwa na Idara ya Fizikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kalanja amesema anaelewa kuwa kufundisha somo hilo na kulifanya lipendwe sio jambo rahisi, bali inahitaji uelewa wa somo, kujituma, uvumilivu, rasilimali fedha pamoja na muda wa kuandaa vifaa mbalimbali vya kufundishia.

Amesema mafunzo kama hayo, yataweza kuwa ufunguo wa mafanikio katika kuongeza idadi na kiwango cha wanafunzi wanaochukua somo hilo na sayansi kwa wingi shuleni na vyuoni.

Naye Mkuu wa Idara ya Fizikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Nuru Mlyuka, amesema mafunzo hayo kwa walimu yalianza kutolewa tokea mwaka 2020 mpaka sasa mara mbili kwa mwaka, lengo likiwa ni kutoa mbinu hizo, ili wanafunzi waelewe na kupenda somo hilo.

“Kinachofanyika ni mbinu mbalimbali za kuhakikisha kuwa kila mtoto anashiriki kwenye kujifunza, sio wengine waachwe wengine ndio washiriki,” amesema.

Amesema Tanzania inataka kujenga uchumi wa sayansi na teknolojia kuelekea uchumi wa viwanda, ili kupata wataalam hao ni lazima kuanzia kwa vidato vya chini, ili watoto wayapende masomo na kufaulu.

Mwalimu Aveline Chugulu kutoka Sekondari ya Minazi Mirefu, amesema mafunzo hayo yanatoa mbinu kwa walimu, ili waweze kuwafundisha wanafunzi kutoogopa masomo ya fizikia.

Habari Zifananazo

Back to top button