‘Tumieni vituo vya umahiri kutoa mafunzo kwa wachimbaji’

WIZARA ya Madini imeendelea kutumia vituo vya umahiri kutoa elimu na mafunzo ya kisasa kwa wachimbaji wadogo.

Miongoni mwa mafunzo hayo ni uchimbaji wa madini, uyeyushaji wa madini na faida za uwepo wa madini nchini, kupitia vituo vilivyojengwa Kagera, Bariadi, Musoma, Chunya, Songea, Mpanda na Handeni.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema hayo wakati wa ziara yake mkoani Kagera, alipotembela kituo cha umahiri kilichojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.08 na kujionea namna wachimbaji wadogo wa madini wanavyopata elimu na kujengewa uelewa.

Licha ya kuridhishwa na mafunzo yanayotolewa na kituo icho mkoani Kagera, amewasisitiza watumishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Kagera kuwa waadilifu na wazalendo katika uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yao.

Aliwataka watumishi hao kukitumia kituo hicho kuwa mfano bora hata kwa mikoa ya jirani, ambayo haijabahatika kuwa na wataalamu wa kutoa mafunzo ya uchimbaji , kujua namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji madini.

“Hatuwezi kusimamia Wizara ya Madini kama hatuna weledi, uadilifu na uwajibikaji na tukizingatia kwamba sekta hii ndiyo inayoongoza kwa kuuza bidhaa zitokanazo na madini nje ya nchi, vituo vyetu vilivyojengwa ni bora sana na ninajua mnavyowapokea watu wengi kwa ajili ya kuwapa maarifa basi kituo hiki kiendelee kutumika vizuri na kuleta faida kwa nchi yetu, ” alisema Mbibo.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kagera, Samwel Shoo alisema kuwa mkoa Mkoa wa Kagera una lesseni za wachimbaji wadogo 811, lesseni za wachimbaji wakubwa 2, lesseni za utafutaji madini 57, lesseni za uyeyushaji madini 2 pamoja na lesseni za wafanyabiashara wa madini 31.

“Shughuli za uchimbaji wa madini zinazidi kuimarika mwaka hadi mwaka, ambapo kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa madini unaofanywa mkoani Kagera  ni madini ya dhahabu, bati ghafi na madini ya ujenzi, ambapo kituo hiki cha umahiri kimekuwa kikiendelea kutoa mafunzo na uzoefu mkubwa kwa wachimbaji wetu wa madini, “alisema Shoo.

Pamoja na mafanikio hayo,  alisema ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vyombo vya usafiri kama magari na pikipiki, vitendea kazi kama kompyuta na samani za ofisini pamoja na upungufu wa rasilimaliwatu.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button