KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche anabeba dhamana ya kuiongoza timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwenye fainali za mataifa ya Afrika zinazotarajia kuanza kutimua vumbi Ivory Coast Januari 13.
Ni dhamana kubwa amekabidhiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) baada ya kuona ana vigezo vyote vya kitaaluma kuwapo hapo.
Alitangaza majina ya wachezaji 31 ambao amesafri nao kuelekea Misri ambapo watacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Misri keshokutwa na ambao atautumia kupata orodha yake ya mwisho kwa ajili ya fainali hizo.
Amepewa dhamana na watu waliopewa dhamana na taifa, hivyo Watanzania hawana budi kumsapoti kama wanatakiwa kufanya jambo na pengine kujiwekea rekodi kwenye fainali hizo.
Pengine kwanini tunasema kujiwekea rekodi kwa sababu Taifa Stars katika ushiriki wake wote haijawahi kupata ushindi wowote kwenye hatua ya makundi. Pengine safari hii inaweza kulifanikisha hilo kupitia Amrouche.
Tanzania ilishiriki mara ya kwanza mwaka 1980 Lagos, Nigeria kabla ya kufanya hivyo mara ya pili katika fainali zilizofanyika Cairo, Misri na fainali za mwaka huu za Ivory Coast ni mara ya tatu.
Hakuna nafasi ya kuhoji uteuzi wake wa kikosi na silaha pekee Watanzania waliyonayo ni kuwa nyuma yake na kuwaunga mkono askari atakaowateua kwa ajili ya michuano hii zaidi ya kumuunga mkono.
Tumeona na kusoma baadhi ya wadau wa soka hapa nchini wakitaja majina kadha wa kadha ambayo wangependa kuyaona yakivuja jasho kwenye fainali hizi lakini kwa bahati mbaya yameshindwa kumshawishi kocha Amrouche kuwajumuisha, ni maoni tu lakini kocha ndiye mwenye dhamana na ameona hao aliowateua mpaka sasa ndio wanaoweza kutimiza malengo yake.
Kinda anayekipiga kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Kelvin John, mshambuliaji chipukizi, Clement Mzize na beki wa kushoto, Nickson Kibabage wote wa Yanga ni baadhi ya majina ambayo baadhi ya mashabiki wa soka wa Tanzania wanahoji kwanini Amrouche hakuyajumuisha kwenye orodha yake hata aliyokwenda nayo Misri.
Katika idadi kubwa ya wachezaji ambao Amrouche amewatumia kwenye michezo mbalimbali iwe ya kufuzu kwa ajili ya fainali hizo ama ya kirafiki nyota hao wanaolalamikiwa na wadau na wengine walikuwepo.
Lakini kitendo cha Amrouche kutowaita kina tafsiri moja tu, ameona kwa wakati huu hawawezi kumfanyia kazi yake kule Ivory Coast ila hawa aliowateua.
Wadau hawana sababu za kiufundi kuhoji uteuzi huu kumzidi mkuu mwenyewe wa benchi la ufundi ambao ndio hasa amepewa dhamana.
Ni jukumu la wachezaji wote waliotemwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kurejea kwenye klabu zao na kupata majibu ya kwanini wameshindwa kumridhisha Amrouche kuwajumuisha na njia pekee ni kufanyia kazi upungufu wao na kuongeza viwango.
Kukaa upande wa kulalamika kwanini hawajaitwa hakutasaidia maisha ya soka ya nyota wote ambao hawajachaguliwa na kocha Amrouche ila kuwaambia ukweli waongeze viwango vyao.