‘Tunafuatilia bei ya korosho soko la dunia’
BODI ya Korosho nchini (CBT), imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya korosho soko la dunia na kutoa taarifa, ili wadau wote waweze kufahamu kinachoendelea katika soko hilo.
Kaimu Mkurungezi wa CBT, Alfred Francis, amesema kuwa hatua hiyo itasaidia wakulima wa korosho nchini kufanya uamuzi sahihi katika biashara ya korosho kupitia minada na soko la awali.
Francis ameeleza hayo ikiwa ni siku chache tangu kuanza kwa minada ya korosho nchini kwa msimu wa mwaka 2022/2023.
Katia minada hiyo ambayo ilianza kwa Mkoa wa Mtwara na Lindi, wakulima wa Korosho katika mikoa hiyo walikataa kuuza Korosho zao kwa bei ya juu ya Sh 2,200 na bei ya chini 1,480, kwa madai kuwa bei hiyo ni ndogo kulinganisha na gharama ya uzalishaji.
Francis amesema kushuka au kupanda kwa bei katika soko la korosho, karanga kwa soko la India, China, bara la Ulaya na Marekani ambao ndio walaji wakubwa, kunasababisha kutoimarika kwa bei ya soko la korosho ghafi.
Ameeleza kutokana na ongezeko la kila mwaka la uzalishaji wa zao hilo duniani, kumechangia kushuka au kupanda kwa soko, ambapo uzalishaji umeoongezaka kutoka tani milioni 1.4 mwaka 2010 hadi tani million 4.1 mwaka 2021.
Amesema upande wa bara la Afrika umeongeza hadi kufikia nchi 20 na uzalishaji kufikia tani million 2.3 kutoka tani 900,000 miaka kumi iliyopita.
Amesema serikali kupitia Bodi ya Korosho itaendelea kusimamia minada hiyo na kutoa elimu kwa wakulima juu ya mwenendo wa soko la korosho ulimwenguni na kuwapa vipaumbele wakulima kufanya uamuzi sahihi wa kuuza, ama kutouza korosho zao bila kulazimishwa na chombo chochote.