‘Tunahudumia wagonjwa 60 wenye kibiongo kwa mwaka’

WAGONJWA  60 wenye matatizo ya kibiongo hufika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Akizungumza mapema leo jijini Dar es salaam, kwenye kambi ya upasuaji wa kunyoosha migongo iliyopinda  ‘vibiongo’ kwa watoto  inayoendelea  MOI, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Dk, Respicious Boniphace, amesema wanapokea wagonjwa wanne hadi watano kwa mwezi na kwa Mwaka wanapokea wagonjwa 50 hadi 60 hali inayobainisha uwepo wa tatizo hilo hapa nchini.

Amesema kuwa wamepokea wataalam ngazi ya Profesa kutoka nchini Marekani na Italia ambao wanaongoza majukumu hayo ya kufundisha madaktari na watakuwepo hadi Aprili 29, 2023.

Ameongeza baada ya mafunzo hayo wataendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa wapya na wengine ambao walifika MOI awali, lakini hawakupata matibabu.

“Wagonjwa wenye umri wa chini ya miaka 10 tiba yake ni rahisi kwani hawafayiwi upasuaji na badala yake  atapatiwa tiba rahisi, inaepusha gharama,” amesema.

Amewasihi wazazi kuwawahisha watoto wao pindi wanapoona dalili za kibiongo ikiwemo kupinda mgongo

Kwa upande wa baktari Bingwa wa Mifupa MOI, Dk Bryson Mcharo amesema, lengo la upasuaji huo ni kujenga uwezo wa madaktari wa taasisi ili kutoa huduma bora kwa wenye changamoto hiyo.

“Katika kipindi hicho cha mafunzo maalum,  MOI wanatarajia kuwafanyia upasuaji wagonjwa watano hadi sita chini ya wataalam wanaoongoza mafunzo hayo kutoka Marekani na Italia,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button