HATUNABUDI kulipongeza Bunge kwa kuridhia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa uendeshaji wa bandari nchini baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai
Tunawapongeza wabunge kwa kuchua hatua hii muhimu kwa mustakabari wa nchi hasa katika ukuaji wa uchumi.
Tunasema ni hatua muhimu kwa kuwa serikali kupitia kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ushirikiano huu utaleta manufaa muhimu mkubwa ikiwamo ongezeko la mapato, ajira na idadi ya meli nchini.
Profesa Mbarawa anasema Tanzania itapata manufaa zaidi ya 14, jambo ambalo kwa Watanzania wapenda maendeleo hawanabudi kusapoti hili.
Wabunge jana waliridhia Mapendekezo ya Mkataba baina ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji kazi wa bandari Tanzania.
Tunaamini, makubaliano hayo yatafungua fursa pana kwa Tanzania kuongeza ufanisi wa bandari nchini.
Tunaungana na wadau mbalimbali wa bandari ambao wameonesha kuridhishwa na hatua hii ambayo inakwenda kuinufaisha nchi.
Kumbuka katika manufaa yaliyotajwa na Profesa Mbarawa, ni ajira na meli kuongezeka.
Kwa hili la ajira, tunaamini lina mchango mkubwa katika utatuzi wa vijana wengi ambao wangependa jambo hili liive mapema zaidi waweze kuingia kazini.
Mbarawa anasema pia kutakuwa na ongezeko la mapato ya serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Sh trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi Sh trilioni 26.7 mwaka 2032/33 sawa na ongezeko la asilimia 244.
Hili nao ni jambo kubwa ambalo Watanzania walione. Nchi yoyote duniani inategemea ukusanyaji wa kodi katika kila nyanja.
Tunachoweza kusisitiza kama baadhi wabunge na wadau wa bandari walichoshauri, ni kuwa makini katika kuandaa mikataba ili iwe na tija kwa nchi.
Ikumbukwe Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza hili la mikataba. Wanasheria wetu waliobobea katika mikataba ya kimataifa waingie kazini ili manufaa ambayo Waziri Mbarawa ameyaahinisha yaweze kuonekana.
Angalia manufa ambayo nchi inakwenda kuyapata likiwamo la kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku tano kwa sasa mpaka saa 24.
Pia kutakuwapo na kupunguza gharama za utumiaji wa bandari, itaongeza idadi ya meli zitakazokuja Bandari ya Dar es Salaam ambapo Waziri anasema zitoka meli 1,569 kwa mwaka 2021/22 mpaka meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
Pia Mbarawa akasema kutapunguza muda wa ushushaji wa kontena kutoka siku 4.5 mpaka siku mbili; kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 mpaka saa moja.
Profesa Mbarawa akasema kutaongezeka shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33 sawa na ongezeko la asilimia 158.
Pia kutaanzishwa maeneo maalumu ya kiuchumi vikiwamo viwanda na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Amezungumza mengi likiwamo la kuchagiza shughuli za viwanda na biashara, ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli kama SGR.
Lakini pia serikali imechukua tahadhari juu ya ukomo wa mikataba ya uendeshaji wa shughuli za bandari.
Profea Mbarawa akatoa hofu wale wenye dukuduku ya muda wa mkataba kwa kusema mkataba wa mradi utakaoandaliwa chini ya makubaliano hayo, utapewa muda wake wa utekelezaji na kuwahakikishia Watanzania kuwa hakuna mkataba wa miaka 100 kama ilivyodaiwa awali katika mitandao.