MTWARA; Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Balozi Ombeni Sefue amesema watahakikisha rasilimali inayotokana na gesi asilia inatumika kubadili maisha ya watu.
Hayo yamesemwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ilipotembelea viwanda vya uzalishaji na uchakataji na gesi asilia vya Mnazi Bay na Madimba vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
Balozi Sefue amesema rasilimali hiyo inatumika kubadili maisha ya watu, pale ambapo gesi asilia inapatikana na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa.
‘’Sisi tumefarijika sana kupata fursa hii ya kuwaonesha wawakilishi wa wananchi fedha za taifa hili katika sekta hizi zinavyotumika na mchango ambao tunatoa katika uchumi wa nchi, kama mlivyosikia karibu asilimia 65 ya umeme unaotokana na gesi inatoka hapa na nyingine inatoka kule Songosongo,‘’ amesema.
Amesema jukumu hilo walilokabidhiwa ni kubwa kwa ajili ya uchumi wa taifa na maendeleo ya wananchi, hivyo wamefurahi kwamba wawakilishi hao kupitia kamati hiyo wamelihakikishia bunge hilo, TPDC, wananchi na serikali kwa ujumla kuwa watahakikisha rasilimali hiyo inatumika kubadili maisha ya watu pale ambapo gesi hiyo inapatikana.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deus Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Sh bilioni 104.6 katika miradi ya gesi asilia nchini, ambayo inaleta manufaa zaidi kwa nchi na kukuza uchumi.
Hata hivyo, imefanya jitihada nyingi hasa uwezaji uliyofanyika wa kuongeza hisa kwenye sekta hiyo huo ambapo kwa sasa Tpdc inamiliki asilimia 40 kutoka asilimia 20 za hapo awali na asilimia 60 zinabaki kwa mwekezaji.
‘’Uwekezaji huu sasa unamfanya TPDC aingie kwenye uzalishaji ambao utakuwa na tija kubwa sana kwa sababu tunajua kwamba asilimia 65 ya umeme kwenye gridi ya Taifa unategemewa kuzalishwa kutoka chanzo cha gesi asilia,’’amesema Sangu