MATUKIO ya hali mbaya ya hewa yanatajwa kuongezeka duniani kutokana na wastani wa ongezeko la joto kufikia nyuzi joto 1.15
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Pwani, katika warsha inayofanyika mkoani humo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Dk Ladislaus Chang’a, amebainisha kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, hivyo waandishi wa habari wakipewa maarifa watakuwa msaada mkubwa kupambana na hali hiyo.
Amesema dunia inapaswa kupambana ili kuhakikisha hali hiyo haiongezeki na kufikia wastani wa 1.5 ifikapo 2030 kama inavyokadiriwa.
Amesema dunia kwa ujumla wake inapaswa kupambana kuepuka kufika wastani wa ongezeko la nyuzi joto 2, hali ambayo itasababisha kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa.
Akizungumzia mafunzo kwa waandishi wa habari, amesema suala hilo kwa TMA limekuwa msaada mkubwa kwa mamlaka hiyo pamoja na serikali kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kujiandaa kuchukua hatua kabla ya majanga.
Akitoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa kiwango cha mvua, amesema upo uwezekano wa mvua kunyesha kwa siku moja na kuvuka wingi wa mvua iliyonyesha kwa mwezi mzima.
“Mvua inaweza kunyesha kwa saa 24, ikawa nyingi na kuzidi kiwango ambacho kimenyesha kwa mwezi mzima, mfano wastani wa mwezi katika mkoa wa Mtwara ni milimita 201, lakini kuna siku ilinyesha na kufikia milimita 369.9 kwa saa 24,” amesema Dk Chang’a.
Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania TMA, imekuwa na utaratibu wa kuwaelimisha waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya hali ya hewa, wakiamini kuwa waandishi ndio njia sahihi ya kufikisha ujumbe kwa wahusika na hivyo kuepusha majanga yanayoweza kutokea.