‘Tutaendelea kushirikiana ili kukuza uchumi’

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), itaendeleza na kuimarisha ushirikiano na serikali ya Muungano wa Tanzania katika nyanja mbalimbali, zikiwemo sekta ya kilimo, utalii, na biashara, ili kukuza uchumi wa pande zote mbili za muungano.
Hayo yamesemwa Waziri wa Klimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa SMZ , Shamata Shaame Khamis mjini Morogoro, wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge inayosimamia Kilimo, Biashara na Utalii kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Kamati hiyo ilikutana na kufanya mazungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa pamoja na sekreterieti ya mkoa huo na kutembelea Kituo cha Utafiti cha Kilimo (TARI) Dakawa,wilayani Mvomero kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali hususani kilimo cha mpunga.
Khamis amesema wizara yake imeweka mkakati maalumu kwa kuhusisha watendaji wa pande zote mbili za Muungano kutoka wizara hizo kwa mujibu wa maelezo ya viongozi wakuu walioelekeza kuwa na ushirikiano na vikao kati ya wizara na taasisi nyingine .
“Viongozi wetu wanatupa ushirikiano na hata tulipoomba ruhusa ya kuja huku (Morogoro), viongozi wetu waliridhia maana yake ni kwamba wanataka mabadiliko na mabadiliko hayo ni kwenye uzalishaji kwenye sekta zetu za kilimo za pande zote mbili,” amesema.Naye Mkuu wa Mkoa ,Fatma Mwassa, ameipongeza kamati hiyo kutembelea Mkoa wa Morogoro, ili kujifunza mambo mbalimbali hususani kilimo cha zao la mpunga.
Amesema kuwa zao la mpunga ndiyo zao kubwa la kimkakati na Tanzania kwa ujumla, kwani mkoa kwa sasa unashika nafasi ya kwanza kwenye uzalishaji wa mpunga nchini.