‘Tutaendelea kusimamia ustawi wenye ualbino’
DODOMA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan itaendelea kulinda na kusimamia haki za Watu wenye Ualbino nchini ili kuwezesha kundi hilo kuwa na ustawi mzuri.
Kauli hiyo imetolewa alipokutana na Wabunge wa Viti Maalum kundi la watu wenye Ulemavu, Viongozi wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) pamoja na Foundation for Disabilities Hope (FDH) kwa lengo la kujadili na kufuatia tukio la kuibwa mtoto mwenye Ualbino lililotokea katika Kata na Tarafa ya Kamachumu Wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Aidha, Ndejembi amebainisha kuwa Utaratibu wa kulinda Watu wenye Ulemavu katika ngazi ya kitongoji, kijiji, kata na wilaya utaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote.
Kadhalika, Ndejembi amewataka Watu wenye Ulemavu kutokuwa na hofu kwa kuwa Vyombo vya Ulizi na Usalama vitaendelea kudhibiti vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakao bainika kufanya matukio hayo. Pia, amepongeza jitihada zinazofanywa na uongozi wa Mkoa wa Kagera, Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na wananchi katika harakati za kumtafuta mtoto huyo.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum Stella Ikupa ameishauri Serikali kuwa na mpango na mikakati endelevu ambayo itasaidia kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Foundation for Disabilities Hope (FDH), Michael Hosea amesema kuwa ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuchukua hatua kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu.
“Sisi kama Watu wenye Ualbino tunamatumaini makubwa sana na Serikali kwamba itachukua hatua za kukabiliana na jambo hili,” amesema Hosea.