‘Tutaendelea kushirikiana kwenye michezo, utamaduni’

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dk Pindi Chana ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika uendelezaji wa sekta hiyo.

Amesema hayo leo Machi 29, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania, Suo Peng akieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika kubadilishana uzoefu wa wataalam wanaoweza kutoa ujuzi kwenye sekta hizo.

“Tumekutana leo kuona namna tunavyoweza kuja na ubunifu na kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania na China kwenye sekta zetu hususani maeneo ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutambua kuwa China ina utajiri mwingi kwenye sekta hizi.” amesema Balozi Dk Pindi Chana.

Amesema Tanzania na China zimekua na ushirikiano mkubwa katika masuala mbalimbali tangu uhuru ambapo viongozi waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Tse Tung wa China walianzisha ushirikiano huo kwa manufaa ya Wananchi wa pande zote akiongeza kuwa China imekua ikitoa misaada mingi kwenye maeneo mbalimbali.

Waziri Balozi Pindi Chana ameeleza kuwa Tanzania na China zimeshaingia na kusaini makubaliano ya uendelezaji wa masuala mbalimbali ambayo pia Marais wa nchi hizo wamekua wakiyaeleza hivyo ni wakati muafaka wa kuendelea kuyatekeleza.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi wa China Suo Peng amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China zimekua na ushirikiano mkubwa tangu miaka ya 1960.

Habari Zifananazo

Back to top button