Tutoe maoni bila jazba miswada ya sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa
KATIKA mojawapo ya falsafa zake za R nne za Rais Samia Suluhu Hassan, zipo mbili zinazozungumzia kuhusu mariadhiano na mageuzi. Falsafa nyingine mbili zinahusu ustahimilivu na kujenga upya.
Katika hotuba yake kwa taifa kwa ajili ya kuukaribisha mwaka huu wa 2024, Rais Samia aligusia kuhusu kasi ya utekelezaji wa falsafa ya R 4 katika mwaka uliopita wa 2023. Alieleza kuwa katika kutekeleza falsafa ya maridhiano, serikali yake iliendelea na utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na majadiliano na wadau wa demokrasia nchini.
Kwa mujibu wake, ili kutekeleza maazimio hayo, tayari serikali imewasilisha bungeni miswada mitatu kuhusu Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa. Na kutokana na kuwasilishwa huko kwa miswada hiyo, Bunge limewaita wadau kutoa maoni yao kuanzia Januari 6, 8, 9 na 10 bungeni Dodoma.
Ni kwa msingi huo basi, tunaamini wadau watajitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kama ambayo taratibu za utungaji wa sheria unavyoelekeza kwa mujibu wa Bunge. Tunaungana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliyetoa wito kwa Watanzania kushiriki katika kutoa maoni kuhusu miswada hiyo mitatu ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia kujenga Tanzania iliyo bora zaidi katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Sisi tunaamini hii ni fursa nzuri katika kujenga demokrasia nchini na pia kuleta mageuzi kama ambavyo Rais Samia amekusudia, hivyo ni wakati mwafaka unaopaswa kutumiwa vyema na wadau ili kujenga taifa kwa misingi ya sheria zilizo nzuri.
Haifai na haitakuwa na tija endapo watu hawatajitokeza na kubaki kulalamika, bali watumie nafasi hii kuisaidia serikali kutimiza azma ya kuwa na sheria hizo tatu bora zilizokusudiwa. Na ni vyema pia kutumia nafasi hii kwenda kutoa maoni yao bila jazba, hila wala kukomoana kwa sababu nia ya serikali ni nzuri, hivyo itatumiwa vizuri na wadau wa demokrasia ili kuunga mkono juhudi kubwa za Rais Samia kuijenga nchi.
Ni wakati wa Watanzania na wadau wa siasa nchini kutanguliza mbele maslahi makubwa ya nchi, kama alivyoeleza na kuahidi Rais Samia katika hotuba yake ya Mwaka Mpya kuendelea kushirikiana na wadau hao. Watanzania na hasa wanasiasa watambue dhima kubwa waliyonayo katika mustakabali wa taifa, wakijielekeza kwenye kujenga taifa na kulifanya liendelee kudumisha umoja na mshikamano na kupigiwa mfano barani Afrika na dunia kwa ujumla.
Wasipoteze nafasi hii muhimu ambayo itasaidia kuimarisha demokrasia nchini na kuendelea kuweka misingi ya kufanya siasa zenye ustaarabu kwa maslahi mapana ya taifa