Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere yazinduliwa Dar

SERIKALI imezindua rasmi tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kwa waandishi mahiri wa riwaya nchini kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/23 na zitatolewa rasmi Aprili 13, 2023.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Septemba 12 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, amesema lengo la kuwa na tuzo hizo ni kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu miongoni mwa jamii.

Pia amesema ni kuwatambua kitaifa waandishi mahiri katika nyanja za riwaya na ushahiri, kukuza lugha ya Kiswahili, kukuza kipaji cha wabunifu, kuhifadhi historia, kukuza sekta ya uchapishaji, kuongeza hifadhi binafsi katika maktaba za taifa na mikoa.

Amesema tayari wizara yake katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23,  imetenga fedha kwa ajili ya utoaji wa tuzo hizo, kama zawadi kwa washindi, ambapo mshindi wa kwanza atapata kitita cha Sh milioni 10, mshindi wa pili atapata Sh milioni saba na mshindi wa tatu atapata Sh milioni tatu.

Amesema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji. “Katika bajeti yetu ya mwaka 2022/23 tumeshatenga Sh bilioni moja ambazo watapatiwa washindi kwa ajili ya kuchapisha na kusambaza riwaya watakazokuwa wameandika na zikashinda, tutazipa ithibati na kusambazwa shuleni,” amesema Prof. Mkenda

Naye Mwenyekiti wa Maandalizi ya Tuzo hizo, Prof. Penina Mlama, akizungumzia tuzo hizo, alinukuu hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitoa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika alisema: “Kujenga taifa si suala tu la kujenga barabara za lami, ghorofa, hoteli za kifahari na kadhalika.

 

Baadhi ya wageni mbalimbali, wakiwemo watunzi mahiri wa riwaya wakishuhudia uzinduzi huo.

“Unaweza kuwa na yote haya, lakini nchi isipate kuthaminiwa, kujenga taifa kwa maana halisi, kazi ambayo sote tunapaswa kujitosa kuifanya kwa moyo wote ni kujenga tabia za watu, kujenga mitazamo itakayotuwezesha kuishi pamoja na wananchi wenzetu wa Tanganyika na ulimwengu mzima.

“Kila taifa limejiwekea mifumo na mitazamo, ili watu wao waweze kuishi pamoja na kuthaminiana,” amesema akinukuu hotuba hiyo.

Amesema mifumo na nyenzo hizo ni pamoja na mitazamo na amani, mifumo inayolinda haki za kila mtu, inayojenga tabia njema.

Amesema tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, imepewa jina hilo kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, ambaye pia alikuwa mwandishi wa mshairi na tenzi pamoja na fasihi, pia alikuwa kiongozi aliyegusa mawazo huru na kuchochea lugha ya Kiswahili katika kuunganisha taifa.

Prof. Mlama amesema kwa kuanzia tuzo hilzo  zitatolewa kwa nyanja mbili za riwaya na kwamba vigezo vya ushiriki ni mwandishi lazima awe raia wa Tanzania, awe mbunifu katika lugha ya Kiswahili, awasilishe andiko bunifu katika nyanja moja tu ama riwaya au ushairi.

Amesema urefu wa riwaya unapaswa kuwa kuanzia maneno 60,000 mpaka 100,000, wakati kwa upande wa mkusanyiko wa mashairi ni kuanzia kurasa 60 na 1,000.

“Muswada usiwe umechapishwa na mchapishaji binafsi, mshiriki anaruhusiwa kushiriki katika andiko moja tu, andiko liwe makini lililojikita katika masuala ya muhimu ya kijamii,” amesisitiza Prof. Mlama

Amesema dirisha la kupokea kazi za wabunifu litafunguliwa rasmi kuanzia kesho Septemba 13, hadi Novemba 30, kupitia barua pepe tuzo Nyerere @ tie.go.tz. na kwamba majaji watapitia kazi hizo kuanzia Desemba hadi Machi 2023 na tuzo rasmi zitatolewa Aprili 13, 2022, ambayo ni siku aliyozaliwa Nyerere

Habari Zifananazo

Back to top button