Tuzo yampa mzuka Barres

KOCHA wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed (Barres) amesema baada ya kushinda tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi Aprili, malengo yake sasa ni kupata mafanikio zaidi akiwa na timu hiyo.

Kocha huyo ambaye alijiunga na Prisons mwezi Februari mwaka huu, amekuwa mkombozi kwa timu hiyo na kuisadia kuondoka kwenye jinamizi la kushuka daraja, ambalo lilikuwa likiwaandama kwa muda mrefu.

Anasema anafahamu ugumu uliopo kuipandisha timu daraja pale inaposhuka, hivyo hatamani hilo litokee.
“Gharama ya kupandisha timu ni kubwa mno, kwa hiyo kuliko kuingia gharama hizo ni bora kupambana kuibakisha timu Ligi Kuu ili kurudi imara zaidi msimu ujao,” amesema.

Kocha huyo ambaye alikuwa kocha bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, amepongeza wachezaji wake pamoja na uongozi wa Tanzania Prisons kwa kumpa ushirikiano uliomfanya kuwa kocha bora April na anaamini anaweza kushinda tena tuzo hiyo, ikiwa morali hiyo itaendelea.

Akiwa na na Wajelajela hao, Barres ameiongoza timu hiyo kwenye michezo saba, michezo sita ya Ligi Kuu na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho la Azam, huku akishinda michezo mitatu , vipigo vitatu na sare moja.
Kwa sasa Tanzania Prisons ipo mkoani Kagera ikijiwinda na mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Mei 14 kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Habari Zifananazo

Back to top button