‘Tuzungumze hali halisi katika uwekezaji’

‘Tuzungumze hali halisi katika uwekezaji’

VIONGOZI wa serikali pamoja na wanasiasa nchini wametakiwa kuzungumza uhalisia wa hali halisi katika uwekezaji ili kutafuta suluhisho katika eneo lenye changamoto.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrick Soragha amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya kuangalia mazingira ya ufanyaji biashara nchini Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Mfano kama kadhia ambayo ilijitokeza soko la Kariakoo, tunaambiwaa kuna maelekezo Rais Samia alishaelekeza lakini ukienda kwenye utekelezaji unakuta vitu viko tofauti.

Advertisement

” Wakati huku wanasiasa  tunasimama kwenye majukwaa tunasema kwamba mambo ni mazuri, Rais anahamasisha mazuri, anahamasisha uwekezaji, sheria zetu tumeshazibadilisha, tumeboresha mifumo lakini kiuhalisia bado,” amesema.

Amesema ni vema kuzungumza uhalisia kwa wawekezai ili upungufu uliopo uonekane na kutafuta suluhu.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uwekezaji kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi amesema kitu ambacho serikali inavutiwa nacho ni kuridhika kwa wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali.

Ameshauri wakati wote kuwe na majadiliano na mijadala ambayo inaimarisha mazingira ya biashara kwa serikali ni sikivu kwa masuala katika uwekezaji yanayoweza kufanyiwa kazi.

“Nchi za Nordic ambazo ni Sweden, Finland, Denmark na Norway ni wabia wa muda mrefu wa serikali katika masuala ya maendeleo tunashirikiana nao katika afya,elimu, mazingira na sasa wanataka kuchukua fursa ya uwekezaji,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na Utafiti, masuala ya Uchumi, Umaskini na Maendeleo ya Nchi ( Repoa), Dk Donald Mmari amesema pamoja na mabadiliko makubwa yaliopo katika sera na maboresho ya sheria, bado kuna vikwazo vinaongeza gharama za uendeshaji wa biashara.

“Zingine zinahusiana na uendeshaji wa masuala ya kikodi, nyingine gharama za uchukuzi na mawasiliano. Pia upatikanaji wa nishati ya uhakika na gharama zake,” amesema.

Amesema hayo ni maeneo ambayo juhudi za serikali zimefanyika lakini kunahitajika uharaka hususan wa utekelezaji wa maboresho yanayoendelea katika sheria, sera za biashara na uwekezaji.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark Afrika nchini Tanzania, Monica Hangi amesema ameungana na Repoa pamoja na balozi za nchi za Nordic kuzindua ripoti hiyo ambayo inaonesha mambo mengi yamebadilika yanayoweza kuvutia uwekezaji nchini.

Balozi wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen amesema balozi za Denmark, Finland, Norway na Sweden pamoja na Repoa wameandaa semina ya biashara katika nchi hizo pamoja na uzinduzi wa ripoti hiyo ya mwaka 2022/2023 jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la semina hiyo ni kusaidia na kujadiliana kuhusu sera zilizopo na jinsi ya kuongeza uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na nchi hizo.