Twiga Stars yamkuna Shime

KOCHA wa timu ya soka ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi dhidi ya Comoro lakini amekiri mechi haikuwa nyepesi.

Twiga Stars ipo mjini hapa kwenye michuano ya Cosafa ambapo juzi iliifunga Comoro mabao 3-0 na kuongoza kundi C ikiwa na pointi tatu, ikifuatiwa na Malawi na Angola zenye pointi moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Comoro haina pointi.

Akizungumza baada ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Madibaz, Shime alisema ana imani kikosi chake kitaendelea kufanya vizuri.

Advertisement

“Katika mchezo wa leo (juzi) tumechezesha wachezaji wengi chipukizi ili kuwapa uzoefu na kuongeza nguvu ili tuweze kuzichanga pointi zitakazotupeleka nusu fainali. Nina uhakika nitatoa mchezaji bora kila  mchezo kutokana na ubora walionao wachezaji wangu wa kucheza, kumiliki mpira na kutoa maamuzi sahihi,” alisema Shime.

Pia alikiri wachezaji wa Comoro walikuwa na nguvu na miili mikubwa kuliko wachezaji wa Twiga Stars lakini kadri muda ulivyokwenda walichoka kwa sababu walianza mchezo kwa kasi.

Baada ya mchezo dhidi ya Comoro, Twiga Stars mchezo wa pili itavaana na Botswana kesho na watamaliza hatua ya makundi Septemba 7 kwa kucheza na Malawi ambao walicheza nao fainali msimu uliopita.