MKUU wa mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa amesema uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza katika shule mbalimbali za msingi katika mkoa huo umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na uhamasishaji uliofanyika kwa wazazi na walezi .
Mwassa amesema hayo katika taarifa yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Angellah Kairuki, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mpango mwaka 2023.
Amesema hadi kufikia Januari 6, mwaka huu wanafunzi 65,786 wa darasa la awali wamekwisha andikishwa wakiwemo wavulana 32,543 na Wasichana 33,243 sawa na aslilimia 93.
Mwassa amesema lengo ni kuandikisha wanafunzi wa Darasa la Awali 70,872 wakiwemo wavulana 34,708 na wasichana 36164.
Kwa upande wa Darasa la Kwanza amesema mkoa umeweka lengo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuandikishwa ni 78,846 wakiwemo wavulana 39,195 na wasichana 39,651.
Mkuu wa mkoa amesema hadi kufikia Januari 6, 2023 wanafunzi walioandikishwa ni 74,578 kati yao wavulana 37,342 na wasichana ni 37,578 sawa na asilimia 94.5.
“ Miongoni mwa wanafunzi hawa walioandikishwa wamo wenye mahitaji maalum na kazi ya Uandikishaji inaendelea hadi Machi 31, mwaka huu “ amesema Mwassa
Mkuu wa mkoa pia ametumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa shule na walimu wakuu kujenga kuboresha na kutunza miundombinu ya shule , kuhakikisha kila shule ina hati miliki ya kiwanja ilipojengwa shule na kkishindikana basi angalau hati miliki ya kimila
Pia amewataka kumaliza syllabus kwa wakati ili kutoa muda kwa wanafunzi kufanya marudi, kuwa na majaribio ya mara kwa mara ndani ya shule nay ale yanayoshirikisha shule jirani.
Katika hatua nyingine amesema mkoa huo ulipokea Fedha kutoka Serikali Kuu kiasi Sh bilioni 6.9 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 345 ili kuwapokea Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2023.
“ Madarasa yaliyokamilika ni 336 na matatu yapo hatua za ukamilishaji , viti na meza tayari vipo kwenye madarasa hayo tayari kwa kupokea wanafunzi wanaoanza masomo” amesema Mwassa
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Angellah Kairuki, baada ya kupokea taarifa hiyo amewataka wakuu wa shule na walimu wakuu kuhakikisha watoto wanapokuwa shuleni wanalindwa ili kuwaepusha kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi yao .
Kairuki amesema walimu wanapokuwa shuleni wanajukumu kubwa la kuwalea wanafunzi ili waweze kufikia viwango vya juu zaidi katika elimu yao.
“ Ni Imani yangu mtaendelea kufanya hivyo na nina amni kwa uwezo wenu katika kuongoza shule vyema mtaweza kuyaafikia yote haya” amesema Waziri huyo.